Kigogo Aliyekiri Kuhujumu Uchumi NIDA Aachiwa


MMOJA wa watuhumiwa wa uhujumu uchumi wa vitambulisho vya Taifa (NIDA), Astery Ndege, amehukumiwa kulipa fidia ya Sh 293,446,400.23 kama hasara aliyosababisha kwa mamlaka hiyo kufuatia kukiri kosa lake hilo.



Ndege aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, ameachiwa huru peke yake huku washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu; Meneja Biashara wa NIDA, Avelin Momburi;  Ofisa Usafirishaji, George Ntalima; Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo wakiendelea kubaki gerezani.



Hatua hiyo imekuja baada ya Ndege kuandika barua ya kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukiri makosa ya kuisababisha NIDA hasara ya zaidi ya Sh bilioni 1.1 yalipopelekea kuingia kwa makubaliano.



Akisoma hukumu hiyo jana Jumanne, Oktoba 8, 2019, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally,  amesema mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni nne kwa mashitaka mawili aliyokiri ya kuongoza genge la uhalifu na kusababisha hasara hiyo na kuongeza kuwa amezingatia kitendo cha mshitakiwa kukiri kosa lake na sheria inayoelekeza mshitakiwa kulipa faini.



Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya, aliwasomea washitakiwa wote mashitaka 50 badala ya mashtaka 100 yaliyokuwa yakiwakabili awali ambapo amedai washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 50, yakiwemo ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri, kughushi, kutoa nyaraka za uongo, kutakatisha fedha na kusababisha hasara kwa NIDA.



Hata hivyo, ni mshtakiwa Ndege pekee ndiye amekiri kutenda makosa ya kujihusisha na genge la uhalifu na kusababisha hasara ya zaidi ya sh. bilioni moja, huku wenzake wakikana mashtaka hayo. Kufuatia kukiri mwenyewe, mahakama ilimtia hatiani.



Wakili Komanya aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mshitakiwa kulingana na makubaliano waliyoingia. Pia amedai mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba kitendo cha kuomba msamaha kitasaidia kupunguza msongamano wa watu gerezani.



Kwa upande wake,  wakili wa utetezi, Godwin Nyaisa,  amedai mshitakiwa hajaisumbua mahakama kwa kuwa amekiri na anajutia kosa lake na tayari amekubali kurejesha sehemu ya hasara kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano yao. Amedai mpaka sasa mshitakiwa amekaa gerezani miezi kumi hivyo, anaomba apatiwe adhabu ya faini.



Katika mashitaka ya kusababisha hasara,  inadaiwa Maimu, Ndege na Ntalima kati ya Julai 19, 2011,  na Agosti 31 mwaka 2015 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam,  kwa udanganyifu walisababisha hasara jumla ya Sh 1,175,785,600.93 kwa NIDA

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad