KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, ana imani kubwa na kiungo wake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu baada ya kurejea kikosini hivi karibuni akitokea kwenye majeraha.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Bandari FC ya nchini Kenya uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 lililofungwa na kiungo huyo fundi.
Ajibu hadi hivi sasa amecheza michezo miwili ya Ligi Kuu Bara kati ya minne huku akitengeneza nafasi moja pekee ya bao lililofungwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa kiungo huyo ameshindwa kuonyesha uwezo wake kwenye michezo miwili ya ligi kutokana na kutokuwa na ‘pre season’ nzuri kwake baada ya kupata majeraha.
Aussems alisema kiungo huyo tayari ameanza kurejesha fitinesi yake huku akiamini kwenye michezo ijayo atazidi kuonyesha kiwango kikubwa zaidi ya alichokionyesha walipocheza michezo ya ligi na Kagera Sugar, Biashara FC na huo wa Bandari.
“Maswali napokea kuhusiana na kiwango cha Ajibu, labda niwaambie ni kati ya viungo bora wenye uwezo wa kuchezesha timu na kubadili matokeo ndani ya dakika 90.
“Kikubwa Kilichosababisha ashindwe kuonyesha ubora wake ni majeraha yaliyomuwekea nje ya uwanja kwa muda mrefu na kusababisha kutokuwa na ‘pre season’ nzuri kwake.
“Na hiyo ilisababisha kukosa michezo miwili ya awali ya ligi, hivyo ninaamini kadiri atakavyokuwa anacheza mechi za ligi, basi atazidi kubadilika na kuonyesha kiwango kikubwa,” alisema Aussems.