Kitu gani Kaseja husema na wachezaji kwenye penalt
0
October 30, 2019
Mlinda mlango mkongwe wa Taifa Stars, Juma Kaseja amefichua maneno ambayo huwa anawaambia wachezaji wenzake wa timu ya taifa pindi wanapoelekea kwenye hatua ya mikwaju ya penalti.
Ameyasema hayo alipokuwa akipiga stori na Big Chawa wa Planet Bongo ya East Africa Radio, ambapo amesema kuwa kabla hajaingia langoni kucheza penalti huwa anawaambia wachezaji wenzake kuwa wasikose penalti akiwa na uhakika ataokoa baadhi ya mikwaju ya wapinzani.
"Mimi katika maisha yangu ya kucheza mpira huwa naokoa penalti nyingi, siri kubwa ni kufanya mazoezi. Ambacho huwa nawaambia wenzangu kwenye penalti 5 wajitahidi wasikose na mimi siwezi kufungwa penalti zote tano lazima nitadaka", amesema Kaseja.
Kaseja ameongeza,"kwahiyo huwa tunagawana majukumu, wao wafunge za kutosha na mimi nitazuia".
Aidha Kaseja amezungumzia kuhusu kukimbiwa na marafiki zake wa karibu baada ya kuachwa katika kikosi cha Taifa Stars, ambao hivi sasa wanarejea kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa kipindi alichocheza kama mlinda lango wa taifa.
"Watu wengi tu walinikimbia baada ya kuachwa kwenye timu ya taifa, unajua unapopata wakati mgumu ndio unawatambua marafiki wa kweli lakini hivi sasa nimerudi nafanya vizuri, kuna baadhi ya walewale wanarudi na kwavile mimi ni mtu mzima najua mazingira hayo, maisha yanaendelea".
Golikipa huyo amejihakikishia namba katika kikosi cha Taifa Stars baada ya golikipa namba moja, Aishi Manula kuumia mwezi Agosti, ambapo ameiongoza Stars kufuzu makundi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia pamoja na kufuzu michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani AFCON yatakayofanyika 2020 nchini Cameroon.
Tags