Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema hadi leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 watu 138 wanaodaiwa kuwa na mashtaka ya uhujumu uchumi wameomba msamaha kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) huku nyaraka za wengine 500 zikiendelea kuchambuliwa.
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 mjini Mpanda wakati akizindua safari za ndege kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Katavi.
Amesema kulikuwa na watuhumiwa 700 walioomba msamaha.
“Leo nilikuwa nazungumza na DPP kuhusu taarifa za watu waliotubu. Mpaka leo wamefikia 138, wamesharudisha baadhi ya mabilioni ya fedha,” amesema Rais Magufuli.
“Walioachiwa wako huru wamekwenda kujumuika na familia zao. Huo ndiyo upendo wa pekee kwa sababu tulitoa msamaha na wao wamepokea na sisi tunashukuru. Hao sasa ni raia wema wahesabike kuwa ni raia wema katika nchi yetu.”
Ameongeza, “Nao wataendelea kuachiwa kadri watakavyokuwa wakirudisha fedha, hizo fedha zitatumika kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.”