Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema wadhamini wa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu wanatakiwa kutoa uthibitisho wa maendeleo ya afya ya Lissu pindi shauri hilo linapoitishwa tena mahakamani hapo.
Lissu na wenzake watatu kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwemo kuandika taarifa zenye maudhui ya uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.
Hayo yamebainishwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kuuliza maendeleo ya Lissu ndipo mdhamini wake, Robert Katula alidai kuwa mshtakiwa huyo bado anaumwa.
Kutokana na kauli hiyo, Wakili wa Serikali, Estazia Wilson ameieleza mahakama kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa hivyo hawawezi kuendelea na shauri hilo hivyo wataendelea kumsubiri Lissu hadi afya yake itakapoimarika.
Hakimu Simba alisema shauri hilo litakapokuja mahakamani hapo mdhamini wa Lissu anatakiwa kuja na uthibitisho wa maendeleo ya afya yake.
“Mdhamini wa Lissu utatuletea uthibitisho wa afya ya Lissu ili tuweze kuweka kwenye rekodi zetu,”alisema Simba.
Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 21 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’
Visit website