Mahakama Yavunja ndoa ya Muna Love


HATIMAYE Mahakama ya Mwanzo Magomeni jijini Dar, imevunja ndoa ya msanii wa filamu nchini, Rose Alphone ‘Muna Love’ na aliyekuwa mumewe, Peter Komu baada ya kudumu kwenye mgogoro mzito tangu mtoto wao Patrick alipofariki dunia mwaka jana.  Kwa muda mrefu, wanandoa hao walikuwa kwenye mvutano wa suala hilo ambapo mbali na talaka, wawili hao walikuwa wakivutana ili kujua hatma ya nyumba inayodaiwa wamejenga walipokuwa kwenye ndoa iliyopo maeneo ya Mwananyamala jijini Dar.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Risasi Jumamosi imezipata, Muna ndiye aliyefungua madai ya talaka mahakamani baada ya kuona mambo yake mengi yanashindwa kuendelea kutokana na kipingamizi hicho cha ndoa. “Si unajua ni muda mrefu Muna hayupo pamoja na Peter? Lakini sasa kipingamizi cha yeye ilikuwa ni suala zima la ndoa yake ya awali, hawezi kuolewa wakati tayari bado ana ndoa inayotambulika kiserikali,” kilieleza chanzo makini.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya kesi hiyo kuunguruma kwa miezi kadhaa, Oktoba 9, mwaka huu mahakama ndio ilitoa uamuzi wa kuivunja rasmi. “Sasa hivi Muna yupo huru, anaweza kuolewa na mtu yeyote kama atapenda, si unajua tena bado analipa kabisa,” kilieleza chanzo.

Gazeti hili lilizungumza na Muna ambaye alikiri kupokea talaka yake kutoka kwa aliyekuwa mumewe huyo na kusema kuwa anamshukuru Mungu maombi yake yamejibiwa na sasa yuko huru. “Mungu ni mwema sana na haki imetendeka maana nilikuwa siko huru, lakini naishukuru sana mahakama imetenda haki, ninachosubiri nipate haki kupitia nyumba ambayo tuliijenga wote,” alisema Muna.

Akiendelea kuzungumza alisema kuwa kutopata talaka yake ilikuwa ni moja ya vikwazo kwake hata kupata mume wa kumuoa ilikuwa ni shida kutokana na kuwa na mtu aliyekuwa nyuma yake na kudai ni mke wake. “Vikwazo nilivyopitia Mungu anajua, maana hata huwezi kupata mume kwa sababu anajitokeza mtu na kudai kuwa wewe ni mkewe jamani hebu nipumzike kwa amani kabisa,” alisema Muna.

Risasi Jumamosi lilimtafuta aliyekuwa mume wa Muna ili kumuuliza kuhusiana na talaka hiyo ambapo alijibu kuwa hana la kusema kwa sababu mahakama imeamua na kwa upande wake hana kipingamizi chochote. “Jinsi mahakama ilivyoamua na mimi napokea, wala sina kipingamizi chochote juu ya hilo,” alisema Peter
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad