Makamu wa Rais atembelea shamba la miti, kampeni Dodoma ya kijani


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameupongeza uongozi wa kambi ya Jeshi Makutupora, wakala wa Misitu Tanzania na Watendaji wa Ofisi yake kwa kuhakikisha miti iliyopandwa mwezi Desemba 2017 inaendelea kustawi.

Samia ameyasema hayo hii leo jijini Dodoma baada ya kutembelea shamba la miti lililopo eneo la Mzakwe katika Kambi ya Jeshi Makutupora ikiwa ni ufuatiliaji wa Kampeni aliyozindua mwaka 2017 ya Dodoma ya kijani.

Amesema azma ya kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani iko pale pale na italeta matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa ambayo hupelekea ukuaji wa kimaendeleo, viwanda na shughuli za kilimo.

“Miti hii imekuwa na kustawi kwasababu ya jitihada zenu za kuimwagilia na kuitunza msikate tamaa endeleeni kuitunza kwa kuwa italeta faida baadae katika mapinduzi ya Kilimo, Viwanda na hata ukuaji wa shughuli za maendeleo,”  ameongeza Makamu wa Rais.

Aidha Makamu wa Rais Samia ameagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha tafiti zinakamilika mapema kutoka katika sampuli ya udongo iliyochukuliwa ili kubaini aina ya miti inayostawi katika eneo hilo na Jiji la Dodoma kwa Ujumla.

Awali Mkuu wa Kambi ya Jeshi ya Makutupora Luteni Kanali Festo Mbanga amesema jumla ya miti 2300 ilipandwa Desemba 21, 2017, ambapo miti 2076 kati ya hiyo imestawi na kukua ikiwa ni sawa na asilimia 90.3 ya miti yote.

“Tumefanya jitihada za kuirudishia miti yote ambayo awali haikuota na tumepanda miti 300 ya ziada na miti inaendelea kustawi na kukua na tunatarajia itaendelea vizuri kwenye ukuaji wake” ameongeza Luteni Kanali Mbanga.

Kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 21, 2017 katika eneo la Mzakwe Jijini Dodoma ambapo jumla ya miti 2300 ilipandwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad