Mambo 5 Yampa Harmonize Ubunge 2020
0
October 20, 2019
‘NI sawa na kumpiga teke chura’ ndivyo tunavyoweza kutafsiri baada ya hivi karibuni Rais Dk John Magufuli kubainisha wazi kuwa angetamani Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ awe Mbunge wa Jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara.
MAMBO MATANO…
Licha ya kauli hiyo ya Rais Magufuli kupokelewa kwa mikono miwili na msanii huyo ambaye unaweza kumuita Harmo, yapo mambo matano ambayo yamedhihirika kumbeba kijana huyo mwenye umri wa miaka 28.
UDHAIFU WA CUF
Jimbo la Tandahimba kwa sasa linaongozwa na Mbunge wa kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Katani Ahmed Katani, chama ambacho tayari kimekumbwa na mpasuko mkubwa ambao umezalisha makundi mawili ya Mwenyekiti Profesa Ibrahimu Lipumba na aliyekuwa Katibu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Tayari Maalim Seif pamoja na wafuasi wake wamekwishahamia Chama cha ACT Wazalendo na kukiacha CUF kikiwa njia panda.
Mbali na udhaifu huo, Harmonize anapata urahisi wa kupenya katika jimbo hilo kwa kuwa lipo chini ya upinzani. Kwa mantiki hiyo CCM nayo inahaha kulirejesha jimbo hilo kwa kuwa lilikuwa linaongozwa na Juma Njwayo kupitia CCM kabla ya kuangushwa mwaka 2015.
KAULI YA RAIS MAGUFULI
Kauli ya Rais Magufuli kuwa anatamani msanii huyo awe mbunge wa Tandahimba ni mojawapo ya mambo yanayombeba Harmonize hasa ikizingatiwa Rais ni Mwenyekiti wa CCM ambaye anaweza kutoa maamuzi ya kulipitisha jina la msanii huyo pindi atakapoona amejitokeza kugombea jimbo hilo ifikapo 2020.
Itakumbukwa kuwa Oktoba 15, mwaka huu wakati akifanya mkutano wa hadhara mjini Ruangwa mkoani Lindi, ambapo Harmonize alitumbuiza na kumkosha Rais Magufuli kiasi cha kuuliza msanii huyo anatokea jimbo gani.
“Lakumalizia… nawapongeza sana waimbaji hawa wakina baba, lakini nampongeza sana Harmonize (Rajab Abdul) sijui anatoka jimbo gani?
“Tandahimba? Mbunge wa kule ni nani?… Aaa ningetamani kweli Harmonize akagombee kule akawe mbunge wa Tandahimba,” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo, katika siku za karibuni Harmonize amekuwa akipewa nafasi ya kutumbuiza katika mikutano mbalimbali ya hadhara anayoifanya Rais Magufuli na kila anapopewa nafasi ya kuimba, Harmonize anaimba wimbo wa ‘Magufuli’ ambao unaelezea mafanikio ya miradi mbalimbali iliyofanywa na kiongozi huyo.
KUSAIDIA JAMII
Hulka ya kusaidia jamii ni mojawapo ya mambo yanayoelezwa kumbeba Harmonize ambapo itakumbukwa Machi 22, mwaka huu, msanii huyo alitoa vitambulisho 200 kwa wamachinga katika soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kuwamwagia pesa za kutosha ambazo haijajulikana ni kiasi gani.
Harmonize aligawa vitambulisho vinavyouzwa kila kimoja Sh 20,000 kwa wafanyabiashara hao ambao pia asilimia kubwa wanaaminika kutoka ukanda wa Mtwara na Lindi.
UMAARUFU
Umaarufu ni mojawapo ya kete muhimu ya mafanikio kisiasa hasa ikizingatiwa sasa wananchi wa Tandahimba watakuwa wanamfahamu vema kijana wao.
UWENYEJI WA TANDAHIMBA
Mojawapo ya jambo linalombeba msanii huyo kutwaa jimbo la Tandahimba ni uwenyeji wake katika jimbo hilo kwani Harmonize amezaliwa katika Kijiji cha Mahuta, Tandahimba mkoani Mtwara.
Uwenyeji huo tayari umeanza kumpigia chapuo ambapo baadhi ya wananchi wamesikika wakimuomba msanii huyo agombee ubunge kwenye Jimbo la Tandahimba
KAULI YA HARMONIZE
Akizungumza na Risasi Jumamosi, Harmonize alisema anamshukuru rais kwa kuona mchango wake kwenye jamii na Mungu akipenda atagombea.
ANACHOTAKIWA KUFANYA
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 67 1(A) na (B) inayoelezea sifa za kuwa mbunge, kuwa awe raia wa Tanzania, anayejua kusoma na kuandika Kiingereza na umri usiopungua miaka 21.
Hizo ni sifa ambazo msanii huyo amezitimiza lakini wachambuzi wa siasa pia wanaonya kuwa msanii huyo kwa sasa anatakiwa kujiepusha na kashfa zinazoweza kumharibia heshima yake kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoshiriki au kuonesha kampeni zozote za kulitaka jimbo hilo mpaka kipenga kitakapopulizwa na CCM.
Tags