SAKATA la wanandugu wa familia ya marehemu bilionea Erasto Simon Msuya, wakazi wa Arusha wanaodaiwa kugombea mali za marehemu, limechukua sura mpya baada ya upande wa baba wa marehemu kuibuka na kudai kwamba hakuna mgogoro bali suala hilo linazushwa kwa maslahi ya upande wa mke wa marehemu.
Pia alikanusha madai ya kufunga nyumba tano za marehemu na kusababisha watoto wa marehemu kuishi hotelini na kudai kuwa mtoto mkubwa wa marehemu aitwaye Kelvin Msuya (22) aliamua kuishi mwenyewe hotelini kwa kupenda na si kwa kufungiwa nyumba.
Akizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita, mama mzazi wa marehemu Erasto, Ndeshu Msuya ameeleza bayana kwamba nyumba hizo zilifungwa kwa sababu ya usalama baada ya mke wa marehemu, Miriam Mrita kukamatwa kwa tuhuma za mauaji ya wifi yake; Anitha Msuya na kukosa mwangalizi kutokana na baadhi ya vitu kupotea.
Alisema hatua hiyo ilikuja kufuatia nyumba aliyokuwa akiishi marehemu na familia yake, upande wa mke wa marehemu kutaka kuiuza kwa kuwa haikuwa sehemu ya mali za mirathi za marehemu zilizokuwa zimeorodheshwa.
Mama Ndeshu alidai kwamba funguo za nyumba hizo zilikabidhiwa kwa ndugu hao wa mke ambao hadi sasa bado wanazo.
Alifafanua kuwa Kelvin ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu alikuwa akisoma nje ya nchi nchini Australia lakini walimrejesha nyumbani bila kumaliza masomo yake ili kumtumia kama mtaji wa kufuatilia mali za marehemu baba yake.
Mama huyo amesikitishwa na hatua ya watoto wa marehemu wapatao wanne kutopewa haki ya mgao wa mali za marehemu baba yao kwani kwa sasa mali hizo zinawanufaisha ndugu wa upande wa mke ambao wamejigawia kusimamia.
“Sisi kama wazazi wa marehemu tunasikitishwa sana kumtumia huyu kijana suala la mali, kwanza wamemkatisha masomo yake na pale hotelini hana mamlaka yoyote zaidi ya kutumwa kwenda kununua vitu vya hotelini sokoni,” alidai mama huyo.
“Nashukuru waandishi wa habari kwa kuingilia kati jambo hili, nina imani nchi itaelewa ukweli. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, (Jerry Muro) namshukuru pia.
“Erasto alikuwa mtoto wangu pekee wa kiume kwenye uzao wangu kati ya watoto saba wakiwemo mabinti sita, mtoto wangu aliuawa Mijohoroni kila mtu anajua kwamba alipigwa risasi nyingi.
“Kilichotokea muda mfupi baada ya kijana wangu kuuawa, mke wake (Miriam) huku ndani alianza kutoa vitu vyote zikiwemo document mbalimbali na kupeleka kusikojulikana.
“Baada ya kumzika kijana wetu tulikaa kikao cha ukoo pale Boma, tukamuuliza mwali (Miriam) utaolewa ama unabaki kwenye boma, akasema atabaki kwenye boma (Nyumbani kwa marehemu Erasto).
“Kikao cha ukoo tulikaa na kuorodhesha mali zote za marehemu kwa kuziona na kuelezwa, tukaviweka kwenye mirathi tukamwandikia Miriam, tukamwambia simamia mji wako kama ambavyo mlikuwa mkiendesha mji na mume wako.
“Lakini baadaye kabla ya kuzika tukaambiwa kuwa baadhi ya vitu yakiwemo mabegi, yamesombwa usiku wa manane na gari aina ya Land Cruise na kupelekwa kusikojulikana.
“Tulimchagua Miriam kama msimamizi wa mirathi ili akusanye na kama kuna madeni alipe na baadaye agawe mali kwa watoto wake wanne na yeye mwenyewe, lakini akaona kama amechaguliwa kuwa mmiliki wa mali na kufanya atakavyo.
“Fedha zilizopo kwenye akaunti mbalimbali za marehemu kwenye benki, marehemu aliacha wosia wa maandishi kuwa iwapo atafariki dunia, wazazi wake wakiwa bado hai, asilimia 40 wagawane wazazi pamoja na dada zake na asilimia 60 ibaki kwenye akaunti kwa ajili ya mke wake na watoto,” alisema mama huyo.
Naye Bahati Msuya ambaye ni dada wa marehemu alisema kuwa wao kama ndugu wa marehemu hawana nia ya kugombea mali za marehemu kaka yao isipokuwa wanachotaka ni watoto wa marehemu wapewe haki ya kumiliki mali za marehemu baba yao.
Alisema mtoto wa marehemu aitwaye Glory Msuya ambaye yupo masomoni nchini Canada ameshindwa kuendelea na masomo yake ya elimu ya juu baada ya ndugu wa mama yake wanaosimamia hoteli na miradi mingine, kukataa kumlipia ada wakimtaka arejee nchini.
Hata hivyo suala hilo lilitatuliwa na Mkuu wa Wilaya Jerry Muro kwa kuamuru kijana huyo na wenzake kurejea katika nyumba ya baba yao ili kuendelea na makazi.
Muro aliagiza pande zote zinazozozana kufika ofisini kwake jana Jumatatu saa nne asubuhi ili kufikia mwafaka wa changamoto zilizojitokeza.
Marehemu bilionea Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 katika eneo la Mijohoroni wilayani, Hai mkoani Kilimanjaro, Agosti 7mwaka 2013.
Marehemu ambaye alikuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, alifanikiwa kuwa na mali mbalimbali ikiwemo vitega uchumi kadhaa magari ya kifahari, nyumba za kisasa, mashamba, migodi, hotel nakadhalika.