Mchungaji wa Kike wa Kutetema Atikisa, Amuita mama Kanumba!


MWANZA: Achana na ule upepo wa kisulisuli uliokuwa gumzo kutoka kwa Mchungaji Dk Getrude Rwakatare ‘Mama Rwakatare’, mchungaji mwingine anayejiita Mfalme Zumaridi wa mkoani Mwanza, ameitikisa Bongo, Ijumaa Wikienda linakushushia habari kamili.



Kabla ya mchungaji huyo kutoka Kanda ya Ziwa, Mama Rwakatare alitawala kwenye mitandao ya kijamii ambapo watu walikuwa wakisambaziana video hiyo inayomuonesha mama Rwakatare akiwaombea mabinti wengi ambao hawana wachumba ili waume wao waletwa na upepo huo maarufu kwa jina la kisulisuli.



WATU BIZE KUTENGENEZA…

Wengine walikwenda mbali zaidi kwa kutengeneza vipande vya video vinavyoonesha wanawake wengi (siyo halisi) wakimkimbiza mwanaume mmoja wakichombeza na neno ‘upepo wa kisulisuli’.



MAMA AFAFANUA

Wengi walijadili juu ya uhalisia wa upepo huo ambapo mama Rwakatare alitoa ufafanuzi kutoka kwenye kitabu kitakatifu cha Biblia kuonesha kile alichomaanisha; kuwaombea wanawake kanisani kwake wapate wenza wa kuwaoa, kasi inayofanana na ya upepo huo wa kisulisuli ndivyo wanaume watakavyofika madhabahuni kwake na kuwaoa.



TWENDE KWA MFALME SASA…

Wakati gumzo hilo likiendelea, vipande mbalimbali vya Mfalme Zumaridi vilisambaa kama moto wa kifuu kwenye mitandao ya kijamii hususan YouTube.



ANACHOKIFANYA

Kwenye video hizo, Mfalme Zumaridi alionekana akiwa kwenye maandalizi ya kuingia kwenye ibada nje ya kanisa lake.

Akiwa amezungukwa na umati, Mfalme anaonekana akianza kutetema mwili wake kisha kuungwa mkono na waumini wote waliopo eneo hilo.



MWENDO WA KIZOMBI…

Baada ya kutetema kwa muda wa sekunde kadhaa, kinachofuata hapo ni Mfalme kuingia kanisani kwa mwendo wa kuyumbayumba kama vile wafanyavyo wale watu ambao si wa kawaida (mazombi).

Mfalme anaonekana akiwa ameshikiliwa na wanaume maalum waliovaa tisheti zenye picha ya mchungaji huyo wakimzuia asianguke wakati akitembea kwa mwendo wa ‘kutetema.’



“Mh! Hii kali jamani, sasa ndiyo mwendo gani, hawa wababa hadi wakimfikisha madhabahuni si watakuwa hoi maana mama mchungaji Mungu amemjaalia mwili,” alichangia mdau mmoja kwenye mtandao baada ya kuitazama video hiyo.



VIDEO NYINGINE…

Baadhi ya vipande vya video vinamuonesha mchungaji huyo akiwaombea waumini wake huku wakati mwingine wakionekana kusujudu kama wafanyavyo waumini wa Dini ya Kiislam.



AMUITA MAMA KANUMBA

Kwenye video nyingine, imemuonesha mchungaji huyo alivyomuita mama wa aliyekuwa mwigizaji maarufu wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa wakidai kumuonesha marehemu.



Kwenye video hiyo, mama Kanumba anaonekana akieleza jinsi ambavyo Mfalme alimshawishi hadi akakubali kwenda jijini Mwanza katika kanisa lake.

“Nilikuwa nikikataa sana maana nilishahangaika mno kuhusu suala la kuoneshwa mwanangu, nilishaenda mpaka kwa TB Joshua huko, lakini sijui ilikuwaje bwana Mfalme akazidi kunishauri hadi nikaja,” alisikika mama Kanumba katika video hiyo.



Mama Kanumba alimshukuru Mfalme Zumaridi kwa kumfikisha hapo ambapo pamoja na mambo mengine, alielezwa jinsi ambavyo wameoneshwa mambo mbalimbali aliyokuwa akiyafanya Kanumba enzi za uhai wake ambapo mama huyo alikiri kuwa ni ya kweli.



IJUMAA WIKIENDA NA MAMA KANUMBA

Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda baada video inayomuonesha akiwa kwa Mfalme Zumaridi kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii, mama Kanumba alifunguka mchezo mzima ulivyokuwa hadi akaenda.



MAMBO YALIKUWA HIVI…

Ijumaa Wikienda: Wewe ulishawahi kwenda kutetema kwenye Kanisa la Mfalme Zamaradi?

Mama Kanumba: Ndiyo nilishawahi kwenda kwa nini nikatae?

Ijumaa Wikienda: Nani alikupeleka kwa huyo mchungaji?

Mama Kanumba: Wao wenyewe walinitafuta na kuniambia kuwa mama njoo mtoto wako yuko kanisani huku.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo uliwaamini?

Mama Kanumba: Unajua nina uchungu na mtoto wangu, hivyo hata mtu akiniambia anapatikana katikati ya Bahari ya Hindi nitaenda tu ili nimpate.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo ni nani alikupeleka?

Mama Kanumba: Walinitumia tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi, nikafikia hoteli waliyoniandalia na kesho yake ndiyo nikaenda kanisani.

Ijumaa Wikienda: Ilikuwaje huko kanisani?

Mama Kanumba: Hapo ndipo nilipowavuruga kwani walikuwa wakiniambia niseme Mfalme Zumaridi, mimi nikawa nasema Yesu, wakaona sifai na baadaye walinitaka niseme nimemuona Kanumba. Kwa kweli hapo nilikataa kwa sababu Kanumba sikumuona sasa nitasemaje hivyo?

Ijumaa Wikienda: Sasa ikawaje?

Mama Kanumba: Ndiyo hivyo, niliwakera, lakini nashukuru tiketi yangu ilikuwa mkononi tayari maana walisema hadi Masogange wanaye hapo kanisani, mimi kesho yake nikaondoka kurudi Dar.

Ijumaa Wikienda: Walikutafuta tena?

Mama Kanumba: Wapi, wanaanzaje wakati mimi sikukubaliana nao?

Ijumaa Wikienda: Haya shukurani mama.

Mama Kanumba: Haya asante.

MFALME ANASEMAJE?

Gazeti hili lilimtafuta Mfalme Zumaridi ambapo kupitia ujumbe mfupi alikiri kuwa ni yeye, lakini alipotumiwa maelezo yote ya mama Kanumba na kuhusu ibada yake, hakujibu chochote.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad