HAKUNA aliye salama! Hiyo ndiyo taarifa kutoka Jeshi la Polisi ambayo imetua kwenye Dawati la Gazeti la Ijumaa Wikienda kwamba, wale wote ambao wamesambaziana video chafu za ngono zinazodaiwa ni za msanii wa Bongo Fleva na mshereheshaji Menina Atick ‘Meninah’, watafikiwa na mkono wa sheria.
GUMZO LILIIBUKA ALHAMISI
Video hizo zinazomuonesha Meninah akiwa anavunja amri ya sita na mwanaume ambaye haonekani sura, zilikuwa gumzo zaidi kwenye mitandao ya kijamii Alhamisi iliyopita ambapo watu mbalimbali walitoa maoni yao. Wengine walimponda Meninah, lakini wengine wapo waliomtetea.
CHANZO KUTOKA POLISI
Kwa mujibu wa chanzo makini kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar, msako mkali wa kiuchunguzi utafanyika ili kuhakikisha wote waliohusika kusambaza picha hizo wanakamatwa na kufikishwa polisi kisha kufunguliwa mashtaka chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao.
“Yaani ni hatari, wapelelezi watawafikia watu wengi sana katika hii kesi maana Meninah amemshtaki mmoja wa wasambazaji wa picha hii, tayari amekamatwa. Sasa kama unavyojua ukifuatilia mlolongo wa watu kusambaziana hauishii kwa huyu mtu pekee aliyekwishakamatwa,” kilisema chanzo hicho.
CHAZIDI KUTIRIRIKA
Chanzo hicho kilizidi kueleza kuwa, watu wote ambao wamesambaziana video hizo wanaweza kufikiwa kirahisi kwani teknolojia inawezesha wao kujua video hii imetumwa kutoka kwenye kifaa gani na kwenda kwenye kifaa cha nani.
“Ni rahisi tu sisi ku-track hadi kuupata mtandao wote. Hivi vifaa kama kompyuta, simu, ipad na vinginevyo, kinapokamatwa kifaa kimoja, kuna uwezekano polisi kuweza kutambua imesambazwa kwenda kwenye vifaa gani vingine pia ni rahisi kumjua mtumiaji wa hicho kifaa hususan katika simu ambapo zote zimesajiliwa,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya Jeshi la Polisi.
TAHADHARI YATOLEWA
Chanzo hicho ambacho pia ni miongoni mwa polisi, kilitumia nafasi hiyo pia kuwaasa Watanzania kuwa makini katika kipindi hiki ambacho Sheria ya Makosa ya Mtandao inafanya kazi kwani bila kujua, muda wowote unaweza kujikuta kwenye mikono ya sheria na una kesi ya kujibu.
“Wananchi wawe makini mno, hiki siyo kipindi kile cha watu kuona tu vitu na kurusha kwa marafiki. Ukiona mtu amekurushia kitu, usisambaze kabisa kwa watu wengine. Unaweza kukuta yule aliyekurushia amekamatwa na wewe ukajikuta umekamatwa vilevile,” alisema polisi huyo.
TUMSIKILIZE KAMANDA KINONDONI
Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu ambapo alipopatikana alikiri kumshikilia mtu mmoja ambaye Meninah anamlalamikia kusambaza video zake chafu mitandaoni.
“Tupo naye polisi tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Kamanda Taibu bila kumtaja mtuhumiwa huyo wanayemshikilia. Hata hivyo, Gazeti la Ijumaa Wikienda lilizungumza na mmoja wa maofisa wa polisi anayehusika na Kitengo cha Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime) wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambaye alimtaja mwigizaji mmoja Bongo ambaye alikuwa swaiba wa Meninah kuwa ndiye wanayemshikilia.
Wakati Gazeti la Ijumaa Wikienda linakwenda mitamboni, yaliibuka madai kuwa Menina amekamatwa na polisi kwa kosa la kusambaza video za lugha chafu kwa viongozi, lakini hata hivyo alipotafutwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa alisema taarifa hizo hazijamfikia mezani kwake.
STORI: NEEMA ADRIAN, DAR