Mgonjwa Afungiwa Ndani kwa Minyoyororo Miezi Miwili


Shadrack Johanes (26), mkazi wa Old Shinyanga, Manispaa ya Shinyanga, amefungiwa chumbani akiwa uchi kwa miezi miwili akiwa amefungwa minyororo mikono na miguu.

Imeelezwa kuwa ndugu wa kijana huyo ambaye amekutwa kwenye chumba hicho akiwa uchi, walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuwa amepata tatizo la akili.



Shangazi wa kijana huyo, Devota Emmanuel, aliiambia Nipashe juzi kuwa baada ya kuanza kupatwa na tatizo hilo la akili, mpwa wake alianza kupiga watu, kuvunja vioo vya magari na nyumba za watu.

Kutokana na kutumia fedha nyingi kuwalipa watu waliokuwa wanaharibiwa nyumba na magari yao na kijana huyo, Devotha alisema waliamua kumfungia ndani ili asiendelee kuwatia hasara.



Alidai kuwa walimpeleka Hospitali ya Rufani ya Bugando jijini Mwanza kupatiwa matibabu, lakini madaktari hawakubaini ugonjwa unaomsumbua, hivyo kuwapa rufani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.



“Kutokana na hali ngumu ya kimaisha na ukosefu wa fedha, tukaamua kurudi naye hapa nyumbani na kumfungia ndani ili asifanye fujo tena mitaani,” Devotha alisema na kueleza zaidi:

“Kijana huyu ni mtoto wa kaka yangu, baba yake yuko Bukoba na ameshakata tamaa, msaada mkubwa nimebaki ni mimi na kaka yake, na sisi hatuna uwezo wa kifedha kumpeleka huko Muhimbili, ndiyo tukaamua kumfungia ndani takribani miezi miwili sasa.



“Tumemfunga minyororo hii ili asitoroke na tukimvalisha nguo ana zichana, ndiyo maana tukaamua kumwacha aishi hivyo akiwa uchi.

“Tumeweka ndoo ya kujisaidia lakini huwa anajisaidia chini na chakula chake huwa ana kula humo humo (chumbani), na mpaka sasa hatujui tufanye nini.”



Kaka wa kijana huyo, Golden Johanes, alisema imekuwa vigumu kwao kumsaidia mdogo wake kutokana na madaktari kushindwa kubaini tatizo linalomsumbua.

Alisema wanaamini huenda mdogo wake huo “amechezewa kishirikina” na kwamba familia yao haina uwezo wa kifedha kumpeleka kwenye matibabu ya kibingwa Muhimbili ndiyo maana ikaamua kumfunga minyonyoro chumbani.



Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga, Panuela Samwel, alilaani kitendo hicho, akieleza kuwa ni ukatili. Aliitaka familia hiyo kumsafisha kijana huyo na kuhakikisha inamvalisha nguo, kumlaza kwenye godoro badala ya sakafuni, kumpatia chakula kwa wakati na kumhifadhi sehemu safi.



Ofisa huyo wa serikali pia aliitaka familia hiyo kuhakikisha ndani ya wiki mbili kuanzia juzi, iwe imeshajipanga kifedha kumpeleka kijana huyo kwenye hospitali zinazotoa matibabu ya ugonjwa wa akili.

Alisema kitendo cha kumficha chumbani na kumfunga minyororo kinaweza kusababisha magonjwa mengine yakiwamo ya mlipuko.



Mei 19, 2014, mtoto mwenye ulemavu wa akili (15) aligundulika wilayani Korogwe amefungiwa ndani ya chumba kwa miaka tisa kutokana na hali yake ya ulemavu.

Ilibainika aliyefanya kitendo hicho ni mama yake wa kambo ambaye alimfungia ndani ya chumba na alikuwa akijisaidia humo haja kubwa na ndogo na kuwekewa chakula katika bakuli maalum.



Pia, Julai 16, 2014, wadau wanaotetea haki za watoto walimtembelea, Apewe Mathayo (12), mtoto mwenye ulemavu wa viungo aliyefungiwa ndani kwa miaka 11.

Mtoto huyo aliokolewa na mkazi wa Kijiji cha Kamagambo, Kata ya Kiruruma, wilayani Karagwe, baada ya kutelekezwa na wazazi wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad