Timu ya Azam FC imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Kocha wao wa zamani Aristica Cioaba.
Cioaba anachukua mikoba ya Etienne Ndayiragije ambaye anatarajia kutangazwa kama Kocha Mkuu wa kudumu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kocha huyo raia wa Romania, aliyewahi kuinoa Azam FC misimu miwili iliyopita, ataanza majukumu yake mara moja tutakapokamilisha taratibu za vibali vyake vya kufanya kazi nchini.
Aidha, kama ilivyokuwa awali Cioaba, mwenye leseni ya juu ya ukocha ya UEFA Pro Licence, amerejea sambamba na Kocha wa viungo, Costel Birsan, aliyekuwa naye awali kipindi anaifundisha Azam FC.
Mara baada ya kuingia mkataba rasmi mapema leo Jumatatu, Cioaba ameishukuru Bodi ya Wakurugenzi na uongozi mzima wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani naye.
"Naushukuru uongozi wa Azam FC kwa kuendelea kuwa na imani na mimi, kikubwa mimi sio mgeni hapa naijua timu, wachezaji wananijua na pia wanafahamu falsafa yangu, jambo kubwa ni kuendelea kuifanya timu kuwa juu pamoja na kushinda mataji," alisema.
Ndayiragije anaenda timu ya Taifa, baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC kuridhia ombi la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanaomuhitaji awe kocha mkuu wa kudumu baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho akiwa kocha wa muda.