Mkulima aliyefungua kesi ya kikatiba kuhusu ukomo wa Urais anatafutwa na mahakama
0
October 03, 2019
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam imemtaka Dezydelius Mgoya maarufu kama Mkulima ambaye alifungua kesi ya kikatiba kuhusu ukomo wa urais kutokea mahakamani siku ya Oktoba10, 2019 kufuatia uwepo wa maombi ya Chama cha ACT Wazalendo ya kujiunga na kesi hiyo.
Maombi ya ACT Wazalendo kujiunga na kesi hiyo yameshindwa kusikilizwa leo chini ya Jaji Dk. Benhaj Masoud kutokana na Mkulima kutokuwepo Mahakamani.
Kutokana na kutokuwepo kwa Mkulima leo, Mahakama imekitaka Chama ACT Wazalendo kutangaza wito wa kumuita mahakamani kwenye magazeti mawili yanayosomwa na wengi.
Awali ndani ya Mahakama, Wakili anayekiwakilisha Chama hicho, Jebra Kambole alieleza mbele ya Jaji Dk. Masoud kuwa mara ya mwisho walipokwenda mahakamani hapo walichukua wito wa kumuita Mgoya lakini walishindwa kumfikia kwa sababu hawakujua ana kaa wapi.
Wakili Kambole alidai kutokana na unyeti na uharaka wa jambo hilo, wanaweza kumtangazia wito huo kwenye gazeti ili naye aweze kwenda kusikiliza.
Baada ya kutolewa kwa hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Daniel Nyakiha naye aliiomba Mahakama iwape muda wa siku saba ili kama wana hoja zozote za kupinga maombi ya ACT- Wazalendo waziwasilishe .
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Masoud aliwapa siku saba upande wa mashtaka ili kama watakuwa wana hoja zozote za kupinga maombi hayo watoe majibu yao ndani ya hizo siku hizo.
Pia alikubali Mkulima atangaziwe wito kwenye magazeti yanayosomwa zaidi ili Oktoba 10, mwaka huu afike mahakamani hapo kuisikiliza shauri hilo.
Aidha Jaji Masoud alisema Mkulima huyo apewe nyaraka ili na yeye kama ana utetezi wowote autoe juu ya ACT- Walendo kujumuishwa kwenye shauri hilo.
Nje ya mahakama
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kuwa chama hicho kimeomba kujiunga na kesi hiyo ili kuilinda na kuitetea Katiba.
Zitto alisema kwamba Katiba ya sasa, licha ya mapungufu yake, inapaswa kuheshimiwa ikiwemo uwepo wa ukomo wa urais.
Aidha alisema ni wajibu wa chama chochote cha siasa pamoja na mambo mengine kuhakikisha kinalinda katiba na wao wanaona kesi hiyo ilifunguliwa inaweza kuleta shida za kikatiba.
ACT- Wazalendo wamewasilisha maombi Mahakamani hapo wakiomba kujumuishwa katika kesi hiyo ya kikatiba iliyofunguliwa na mkulima ambaye anahoji kuwepo kwa kikomo cha Urais nchini.
Maombi hayo yaliwasilishwa Septemba 30,2019 kwa Jaji Kiongozi wa Tanzania Dk Eliezer Felesh wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya maelekezo maalumu ya namna ya usikilizwaji wa pingamizi la awali la serikali dhidi ya kesi hiyo.
Maombi hayo yaliwasilishwa na bodi ya wadhamini ya chama hicho inayowakilishwa na kampuni ya uwakili ya Law Guards Advocates chini ya hati ya dharura, wakiomba yasikilizwe haraka.
Katika kesi hiyo ya Msingi, Mgoya alifungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha sharia ya utekelezaji haki na wajibu, sura ya 3ya mwaka 1994 chini ya Ibara ya 30(3) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo Mgoya anahoji Ibara ya 40(20 ya Katiba ambayo imeweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano(10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.
Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42(2) ya Katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13,21 na 22 za Katiba hiyo. Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.
Tags