KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, amezima tetesi za kudaiwa kutaka kuondoka ndani ya kikosi hicho kwa kusema kuwa kwa sasa akili yake inafikiria kutimiza malengo aliyopewa na uongozi huo chini ya mwekezaji, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Aussems ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa za kupewa ofa na Klabu ya Nkana ya Zambia na AS Vital ya DR Congo ambazo zote zimeonyesha nia ya kutaka huduma yake kutokana na rekodi yake ya msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa hana mpango wa kutaka kuondoka Simba kwa sasa kutokana na kuwa na mipango mizito aliyokubaliana na uongozi wa timu hiyo.
“Unajua watu wanasema sana na uzuri nalijua soka la Afrika kwa sababu kila timu inahitaji kuwa na mwalimu mzuri ambaye anaweza kuwapa mafanikio, sasa siwezi kuzuia mtu kuhitaji huduma yangu.
“Lakini kwa sasa wanapaswa kujua bado nina mkataba na Simba ambao utamalizika Juni, mwakani na ukiangalia nina mikakati mikubwa ndani ya Simba ambayo tumekubaliana na uongozi wa timu kuona wapi tunakwenda na hilo kwangu ndiyo jambo kubwa,” alisema Aussems.