Bilionea kijana Afrika na mmiliki wa mojawapo ya klabu maarufu ya soka Afrika mashariki Simba SC – Mohammed Dewji amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu sakata lake la kutekwa nyara mwaka jana na namna alivyotishiwa maisha yake nchini Tanzania.
Katika mahojiano maalum na ya kipekee na BBC Swahili, Mo ameeleza kuwa kwa kipindi kizima, alihisi kwamba kuna uwezekano mkubwa hatoweza kutoka salama na kuwa mwisho wake wa maisha unakaribia.
“Saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi. Imani ndio kitu kikubwa kilichonisaidia katika kipindi kizima.”
Katika kuikumbuka siku hiyo, Mo ameeleza: “Walinifunga macho, miguu na mikono kwa siku tisa. Tulikuwa hatuongei sana, walikuwa sio watu wa hapa.
“Walikuwa wakinitisha na kuniweka bastola kwenye kichwa na kuniambia wataniua.” ameeleza mfanyabiashara huyo.
“Kufunga mlango (wa gari) tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask nyeupe – wamefunika uso, wakapiga bunduki juu mara mbili halafu wameniwekea bunduki.”
Anasema awali alidhani ni jaribio la kutaka kuibiwa gari, na hakuwa na budi kufuata maagizo alipoambiwa alale chini kwenye sakafu.
“Kwenye sekunde sitini hivi, hao watu wamekuja wamenibeba na kuniweka ndani ya gari.”
Anasema kilichofuata katika safari hiyo anayosema iliyokuwa ngumu, watekaji wake walimvua nguo kwa kuhofia huenda ana kifaa cha kutambua anakokwenda yaani tracker na kumfunga mikono na miguu na kwenye dakika 20 wakamfikisha katika nyumba.
“Niligundua kuwa lugha wanayotumia sio lugha ya Tanzania, ilikuwa ni geni.”
“Asubuhi walikuwa wananifungua mikono wananifunga mbele, lakini usiku ndio kulikuwa na mitihani walikuwa wananifunga nyuma. Na wakikufunga nyuma maanake huwezi kulala, lazima ulale kulia au kushoto.”
Mo anasema alikuwa akitoa ushirikiano kwa kila alichotakiwa kufanya. Kikubwa anasema alikuwa akimuomba Mungu atoke salama.
Siku ya tisa anasema “walinisukuma pale Gymkhana na nikasikia gari limeondoka.”
Kwa muda wote alipewa tu kipande cha khanga aliyotumia kujifinika mpaka siku walipomuachilia ndiyo aliyotumia pia kujifunika.
Mo Dewji alitekwa Oktoba 11 2018 na watu wasiojulikana alfajiri wakati alipokuwa akielekea mazoezini alipofika katika hoteli moja ya kifahari katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila siku alfajiri kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.
Siku tisa baadaye, Dewji alirejea nyumbani salama.
-BBC