Mwanariadha wa kike Kutoka Kenya Avunja Rekodi ya Dunia
0
October 14, 2019
Kenya imeendelea kungáa kwenye mashindano ya riadha duniani, siku mbili baada ya Eliud Kipchoge kuweka rekodi ya kuwa binadamu wa kwanza kukimbia Km 42 chini ya saa mbili, mwanariadha wa kike wa nchi hiyo, Brigid Kosgei jana alivunja rekodi ya dunia kwa wanariadha wanawake akiwa jijini Chicago.
Bi. Kosgei mwenye umri wa miaka 25 alivunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Muingereza Paula Radcliffe tangu mwaka 2003. Kosgei alitumia saa 2, dakika 14 na sekunde nne (2:14:04), akiifunika rekodi ya Radcliffe ya saa 2, dakika 15 na sekunde 25 (2:15:25) ya London, Uingereza mwaka 2003.
Katika mbio hizo za Chicago, Muethiopia, Ababel Yeshaneh alishika nafasi ya pili akiwa nyuma ya Kosgei kwa dakika 6 na sekunde 47. Mrembo huyo wa Kenya alionesha uwezo ulioishangaza dunia, ikionesha kuwa kwa mwendo wake angezidiwa na wanaume 22 tu walioshiriki mashindano hayo kwa upande wa riadha za kiume.
Kadhalika, rekodi aliyoiweka Kosgei jana ingeweza kuvunja rekodi ya dunia ya wanaume kama ingekuwa mwaka 1964.
“Ninajisikia vizuri na nina furaha kwa sababu sikuwa natarajia kukimbia kama hivi,” alisema Kosgei baada ya kukamilisha mwendo.
Mwaka jana kwenye mashindano hayo alishinda akiwa amemaliza kwa saa 2, dakika 18 na sekunde 35 (2:18;35).
Tags