Mzee wa miaka 84 abakwa nyumbani kwake, polisi waanza msako
0
October 26, 2019
Ajuza mwenye umri wa miaka 84 anapatiwa matibabu katika hospitali ya Embu nchini Kenya baada ya kuvamiwa na mwanaume mmoja nyumbani kwake aliyempiga na kumbaka.
Polisi wa eneo la Kubugu walitoa fomu maalum kwa ajili ya matibabu (PF3) Alhamisi wiki hii kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ajuza huyo.
Jeshi hilo limeeleza kuwa mtuhumiwa alivamia nyumbani kwa ajuza huyo Alhamisi usiku, katika kijiji cha Ngerwe, Kubugu.
Bibi huyo amewaeleza polisi kuwa mtesi wake alimkokota, akampiga akamziba mdomo kwa kutumia nguo ili kumzuia asipige kelele kabla ya kumuingilia.
Wanafamilia wa bibi huyo wamekaririwa na Citizen ya Kenya wakieleza kuwa walishtuka asubuhi kumuona bibi huyo akiwa na makovu usoni mwake.
Polisi wamesema kuwa wanaendelea kumsaka mtuhumiwa kwani kitendo hicho ni cha aibu na cha kihalifu.
Kumewahi kuwa na ripoti za ubakaji dhidi ya wanawake wenye umri mkubwa (wazee), vitendo ambavyo vilidaiwa kuchochewa na imani za kishirikina hasa Nairobi. Baadhi ya sehemu katika maeneo ya ‘uswahilini’ na vijijini, wazee walipatiwa uangalizi wa ziada.
Mwaka 2015, wazee zaidi ya 200 jijini Nairobi walijumuika katika mafunzo ya kujihami dhidi ya wabakaji yaliyoendeshwa na taasisi ya Thomson Reuters Foundation. Mafunzo hayo yaliitwa ‘Ujamaa self-defense programme’.
Tags