Naibu Waziri Mabula ataka vijana kujifunza maisha ya Nyerere kwa vitendo
0
October 15, 2019
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula amewataka vijana kujifunza maisha ya baba wa Taifa Mwalimu Julius kwa vitendo ili matendo ya kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania yaendelee kukumbukwa.
Akiwa katika Maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu ya Mwl. Nyerere katika kanisa Katoliki la Bikira Maria jimbo la Musoma Parokia ya Butiama mkoani Mara jana Dkt Mabula alisema, ni vyema vijana wa watanzania wakatumia hazina ya wazee kama Mwl Nyerere Julius Nyerere kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo.
"Niwaombe vijana kutumia hazina ya wazee wetu na kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo" alisema Dkt Mabula.
Dkt Mabula ambaye alikuwa Mkuu wa kwanza wa wilaya ya Butiama mkoani Mara alihitimisha salamu zake za miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere wilayani Butiama kwa kuwataka wananchi kuishi pia kwa kumcha Mungu kwa kuwa wakati wa uhai wake baba wa taifa aliishi kwa kumcha Mungu.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba alimueleza Mwl Nyerere kuwa alikuwa ni mtu wa maisha ya Mungu aliyejitahidi kujenga umoja na mshikamano kwa nchi yake na Bara la Afrika kwa ujumla.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Phillip Mangula alimuelezea Mwl Nyerere kama mtu aliyepigania haki na aliyesisitiza kuwa binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja
Tags