Makonda alisema hayo Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na viongozi wa kidini wakati wa kongamano maalumu kuelekea uchaguzi, uchumi wa viwanda, amani, mahusiano, uzalendo na ustawi wa taifa.
Katika kongamano hilo, Makonda alielezea mafanikio ya Mkoa wa Dar es Salaam.
“Ninakosa usingizi, mambo mengi yamebadilika kwa sababu watu wengi si waaminifu, hawana hofu ya Mungu, hawatimizi majukumu yao na hupata kila sababu ya kueleza wamekwama, wengine wanakwama hata kabla hawajaanza.
“Wengine wamekuwa wakitengeneza mabomu ili wenzao walipuke halafu wanakaa pembeni wakishangilia. Na hii ndiyo sababu iliyotufanya mimi na RAS (Ofisa Tawala Mkoa) tumeamua kubadilisha mfumo wa utendaji. Badala ya kuwa watu wa kupokea taarifa ofisini, sisi tunaenda ‘site’ (sehemu za kazi) kutafuta taarifa,” alisema.
Alimweleza mgeni rasmi katika kongamano hilo, Naibu Waziri Tamisemi ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (CCM) ambaye alimwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa jimbo lake barabara imeanza kujengwa, baada ya kuwaweka ndani wakandarasi.
Makonda alisema ni wazi kungekuwa na utamaduni wa watu kuwa waadilifu, kazi zingekuwa zinakwenda vizuri ila kwa kuwa watu wamekosa hofu ya Mungu mambo si kama alivyokuwa akitarajia kwakuwa wengi hawatimizi wajibu wao.
“Kupitia kamati hii, nimeona mafanikio makubwa sana na ninaona kama tungekuwa na utamaduni wa watu kuwa waadilifu, kazi zingekuwa rahisi sana, lakini watu si waaminifu hata kidogo.