Ole Sabaya anavyompa Mbowe, Chadema wakati mgumu wilayani Hai


Julai 28, 2018 Rais John Magufuli alifanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya, mkoa na katibu tawala mmoja akiligusa kundi la vijana. Vijana hao walikuwa ni pamoja na Lengay Ole Sabaya aliyempeleka kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Wengine na wilaya zao katika mabano walikuwa Jokate Mwegelo (Kisarawe), Daniel Chongolo (Kinondoni), Jerry Muro (Arumeru), Patrobas Katambi (Dodoma) na Moses Machali (Nanyumbu).

Mbali na wakuu wa wilaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ally Hapi alipandishwa cheo nja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, huku David Kafulila naye akiteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe. Hawa wote walikuwa ni damu mpya katika ngazi hiyo muhimu ya uongozi katika Serikali za Mitaa.

Ni uteuzi wa kimkakati?

Fikra za baadhi ya watu ziliutazama uteuzi huu kama mkakati wa kisiasa hasa kwenye wilaya ambazo zimekuwa zikionekana kuwa ngome ya vyama vya upinzani.

Miongoni mwa ngome hizo ni wilaya ya Hai ambayo ni jimbo la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hapo ndipo alikopangiwa Ole Sabaya.


Tangu Ole Sabaya ambaye pia ni diwani wa kata ya Sambasha wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, alipoingia wilayani Hai amejidhihirisha kuwa mwiba mkali si kwa Mbowe tu, bali pia kwa Chadema kwa jumla.

Kabla ya tukio la juzi la kiongozi huyo wa Serikali kuagiza askari waingie katika mkutano wa ndani wa Mbowe, kuna mfululizo wa matukio kadhaa yanayoonyesha namna Sabaya anavyoihenyesha Chadema na viongozi wake.

Mbowe anyang’anywa ofisi

Januari 15, 2015, Sabaya alitangaza kuichukua ofisi ya Mbunge wa Hai ambaye ni Freeman Mbowe, akisema itakuwa ikitumiwa na idara ya Uhamiaji, baada ya mbunge huyo kushindwa kuitumia kwa muda mrefu.

Hata hivyo, katibu wa mbunge huyo, Irene Lema alikanusha taarifa ya kupokonywa ofisi ya mbunge wa jimbo hilo kama ilivyotangazwa na Sabaya.

Alisema Mbowe hakuwahi kutumia ofisi yeyote iliyopo ndani ya Halmashauri ya Hai kutokana na kuwa na wageni wengi, huku chumba cha halmashuri kikishindwa kuhudumia idadi ya wageni wengi aliyokuwa nao.

“Mbunge hana ofisi ndani ya Halmashauri ya Hai; aliamua kuweka nje ya halmashauri kwa sababu ilikuwa ni ndogo, hivyo aliamua kuweka nje ya mji ili kuwapokea wageni wengi wanatokea ndani na nje ya jimbo. Hatujawahi kuitumia ofisi ambayo Mkuu wa Wilaya amesema amempokonya Mbunge,” alisema Lema.

Mikutano ya Mbowe yasitishwa, viongozi wakamatwa

Kama hiyo haitoshi, Julai 29, 2019 Jeshi la Polisi Wilaya wa Hai lilimtaka Mbowe kusitisha mikutano aliyopanga kuifanya kwa sababu Sabaya kama mkuu wa wilaya, alikuwa akifanya ziara, hivyo mikutano hiyo ingeweza kuiingiliana. Taarifa hiyo ya Polisi ilisema zuio lingekwisha baada ya ziara ya mkuu wa wilaya.

Kabla ya zuio hilo, Desemba 29, 2018 Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji na viongozi wengine saba wa chama hicho saba walikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro wakati wakiendelea na kikao cha ndani maeneo ya Bomangombe wilayani Hai kwa amri ya ofisi ya mkuu wa wilaya.

Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Basil Lema, alisema kabla hawajakamatwa, Sabaya aliwaandikia barua ya kuzuia kikao hicho, jambo alilosema ni kinyume cha sheria.

Sabaya mwenyewe alikiri kutoa maagizo ya kukamatwa kwa viongozi hao kwa madai kwamba hawakufuata taratibu na kwamba uongozi wa wilaya ulikuwa hauna taarifa.

‘’Ni kweli tumemkamata Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, Katibu wa Chadema Kilimanjaro, Basil Lema, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Helga Mchomvu na msaidizi wa Mbunge wa Hai, Irine Lema, alisema Sabaya kama alivyonukuliwa na Mwananchi.

Aliongeza: ‘’ Naomba nitoe wito kwa wanasiasa kuheshimu sheria na taratibu. Kama mnataka mkutano, kuna taratibu, hamuwezi kuvamia na kufanya mikutano kiholela.’’

Amtumia salamu Mbowe

Septemba 8, 2019 Sabaya, alimtumia salamu Mbowe, akisema muda wake wa kuendelea kuongoza jimbo la Hai umefika ukomo, kwa sababu mambo yote waliyokuwa wanayapigia kelele yamekwishashughulikiwa.

Alitoa kauli hiyo katika kampeni ya Manyara ya kijani iliyozinduliwa mjini Babati na Mwenyekiti wa UVCCM Kheri James, na kusema kuwa kipindi kilichopo sasa si cha kupiga kelele kama ilivyokuwa awali bali ni kipindi cha kumpa nafasi Rais kuendelea kufanya yaliyo mazuri zaidi.

“Mimi nimetumwa na Rais Magufuli kuwa DC wa Hai, lakini nimeteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, mambo ya kuwa ‘neutral’ (kutokuwa na upande) mnayajua ninyi wenyewe. Mimi ni DC na nitawatangazia leo kwamba, kule Hai ufalme umeshafitinika,’’ alisema Sabaya.

Aliongeza kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano ni cha tofauti kwani hata zile kelele za wizi kama vile Escrow, IPTL zilizokuwa zinapigwa na wapinzani kwa sasa hazipo, kwani amepatikana Rais aliyethubutu kurudisha nidhamu ya Serikali.

Mkutano wa Mbowe wavamiwa

Tukio la hivi karibuni ndiyo limeshtua zaidi, baada ya Polisi kuvamia mkutano wa ndani wa Mbowe jimboni kwake. Tukio lilitokea Septemba 30.

Polisi hao wakiongozwa na mkuu wa Polisi wa Wilaya, Lwelwe Mpina walivamia mkutano huo kwa maelekezo ya ofisi ya mkuu wa wilaya.

Sabaya mwenyewe alithibitisha kutuma polisi hao akisema amefanya hivyo kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa Mbowe na viongozi wengine pamoja na wananchi, akisema hawana sababu ya kutaharuki kama ni raia wema.

“Mkutano wa chama cha siasa sio send off au harusi. Mkutano wa chama cha siasa polisi wana haki ya kuwepo. Hata mikutano ya CCM polisi wanakuwepo. Tunafuatilia ajenda ni nini hasa,” alisema Sabaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.

Polisi walifika katika ofisi za Chadema wilaya ya Hai na kulazimisha kuingia ndani ya mkutano huo ili kujua nini kinachozungumzwa kwa lengo la kusimamia ulinzi na usalama kwao na kwa wananchi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad