Prof. Kabudi ataja changamoto zinazoikabili Dunia
0
October 25, 2019
Mabadiliko ya tabia nchi sambamba na matukio ya hali ya kiusalama ikiwemo masuala ya ugaidi na vita ni kati ya changamoto mbalimbali ambazo zimekua zikiikumba Dunia katika utekelezaji wa malengo endelevu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.Paramagamba Kabudi ameyasema hayo jana, Jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya miaka 74 ya Umoja wa Mataifa (UN) yaliyofanyika katika eneo la Nyerere Square.
Amesema baadhi ya Mataifa yamekuwa na matukio mbalimbali kama vile ugaidi, vita pamoja na migogoro mbalimbali ambayo inatakiwa kutatuliwa ili kuweza kurejesha amani kwa baadhi ya mataifa ambayo yamekuwa yakikumbwa na migogoro ya mara kwa mara.
“Tunapoadhimisha mikaa 74 ya Umoja wa Mataifa Dunia inakabiliwa na changamoto mbaimbali za matukio ya kiusalama kama vile ugaidi, vita, migororo mbalimbali pamoja na mabadiliko tabia nchi, na hii inarudisha nyuma utelekezaji wa maendeleo,” amesema Prof. Kabudi.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo Tanzania inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuwa mstari wa mbele kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo ili kuifanya Dunia kuwa sehemu salama na bora ya kuishi kwa wananchi na vizazi vijavyo.
Jumatano Oktoba 23, 2019 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Mnyepe alisema maadhimisho ya miaka 74 ya Umoja wa Mataifa (UN), yafanyika hii leo huku Serikali ikiwa imepiga hatua katika suala la usawa wa jinsia kwa kutoa kipaumbele cha nafasi za uongozi kwa wanawake.
“Maadhimisho haya yana kauli mbiu isemayo Wanawake na Wasichana kuwa kipaumbele kufikia malengo ya Dunia ambapo tayari tumepiga hatua katika usawa wa kijinsia na maadhimisho haya Kitaifa yatafanyika hapa Jijini Dodoma,” alifafanua Dkt. Mnyepe.
Aidha Dkt. Mnyepe alisema wanawashukuru Umoja wa Mataifa (UN) kwa ushirikiano waliowapatia hasa katika kutoa elimu juu ya nafasi ya mwanamke katika uongozi na kuwashukuru wananachi kwa kujitokeza katika viwanja vya Nyerere Square kushuhudia maadhimisho hayo yanayofanyika kwa mara ya kwanza Dodoma.
“Kama Taifa tumekua mstari wa mbele kupigania haki ya mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla hivyo tunaamini katika usawa na nitoe rai kwa watanzania kuendelea kuwaamini wanawake katika mambo mbalimbali kielimu, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi,” aliongeza Dkt. Mnyepe.
Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Balozi Michael Dunford amesema sherehe hizo zimelenga kuhimiza usawa wa kijinsia huku akiipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika utekelezaji wa lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) ambalo linazunguzia usawa wa kijinsia.
Amesema wanaamini kama nchi itafanikiwa katika lengo la usawa wa kijinsia maendeleo endelevu yatapiga hatua kutokana na upande wa Tanzania kufanikiwa katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu na afya na kwamba UN Itashirikiana na serikali katika kufanikisha malengo kusudiwa.
Umoja wa Mataifa umekua ukifanya maadhimisho haya kila ifikapo Oktoba 24 kila mwaka ambapo limefanyika gwaride maalumu la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na bendera ya UN kupandishwa kwa mara ya kwanza Dodoma ikiwa ni Makao Makuu ya Nchi.
Tags