Rais Magufuli azindua uandikishaji orodha ya wapiga kura Serikali za Mitaa 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  hapo jana amefungua barabara ya Sumbawanga – Kanazi, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi, amefungua Kituo cha Afya Nkomolo na kuzindua uandikishaji katika orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (2019) ulioanza leo hapa nchini.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi wa barabara ya Sumbawanga – Kanazi yenye urefu wa kilometa 75 ambayo ni sehemu ya barabara ya Sumbawanga – Kanazi – Mpanda yenye urefu wa jumla ya kilometa 245, uliogharimu shilingi Bilioni 100.7 umekamilika mwaka 2017 na barabara hiyo imekabidhiwa mwaka 2018.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amesema Hospitali ya Wilaya ya Nkasi ambayo inajengwa kwa ghamara ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 500 ni moja kati ya hospitali mpya 69 zenye hadhi ya Wilaya zinazojengwa hapa nchini na kwamba katika bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga fedha za ujenzi wa Hospitali zingine 27 na kufanya jumla ya hospitali zenye hadi ya wilaya zilizojengwa katika Awamu ya tano kufikia 96.


“Mhe. Rais tunakushukuru na kukupongeza sana kwa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kwa miaka miwili tu unajenga Hospitali za Wilaya 96 wakati nchi yetu tangu ipate uhuru ilifanikiwa kujenga Hospitali za Wilaya 77 tu hadi mwaka 2015” amesema Mhe. Jafo katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini Namanyere, Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa.

Kituo cha Afya Nkomolo kilichojengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 500 tayari kimeanza kutoa huduma na kimefunguliwa kwa niaba ya vituo vingine 10 vya Mkoa wa Rukwa ambavyo vimejengwa katika Wilaya zote za Mkoa huo.


Mhe. Rais Magufuli amezindua uandikishaji katika orodha ya wapiga kura wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao umeanza nchini kote leo tarehe 08 Oktoba, 2019 hadi tarehe 14 Oktoba, 2019 na amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowafaa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad