RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amewaongoza Watanzania kupokea ndege mpya ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Boeing Dreamliner 787-8 iliyowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Rais aliwataka Watanzania kutembea kipaumbele kwani ununuzi wa ndege hiyo umethaminiwa hadi na Rais wa Marekani Donald Trump ambaye ametuma salamu zake za pongezi.
Akizungumza wakati wa kupokea ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 262, Rais Magufuli amesema Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limekusanya Dola 14 milioni na kwamba kesho Oktoba 27 ataenda kuhakikisha.
“Tulipoanza kutekeleza mpango wa kuifufua ATCL, baadhi ya watu walidhani tunabeep na wengine walileta vijembe vya chini chini. Tulipoanza kununua ndege zile za Bombadier wapo waliotubeza, lakini sasa wanatuelewa, hongereni sana watanzania, hizi ni kodi zenu, tembeeni kifua mbele, hakuna kinachoshindikana.
“Saa nyingine najiuliza nimewezaje haya, ndiyo maana namshukuru sana Mungu. Jiulizeni kwa nini haya hayakufanyika kabla Magufuli hajakuwepo. Ndege nyingine nne zitaendelea kuja nchini, Bombadier moja itakuja mwezi Novemba 2019 na nyingine mwezi Juni 2020 na Airbus mbili zitakuja Mwezi Juni na Julai 2021.”
“Waziri wetu (Prof. Palamagamba Kabudi) alipokutana na Rais Trump (wa Marekani), Trump ametupongeza kwa kununua ndege Marekani na wakashikana mikono. Hii inaonesha tukinunua ndege kwa wakubwa nasi tunakuwa wakubwa. Tunamshukuru Trump na tunamuahidi tutaendelea kununua ndege Marekani. Chaguo letu ni Boeing.
“Chombo hiki mnachokiona hapa kimeshushwa hapa na Watanzania, fedha zenu zinajulikana hadi Marekani kwamba Watanzania ni matajiri wanaweza kununua kitu kizito kama hiki, siku zote mtembee kifua mbele. Watanzania na Waafrika tunaweza.
“Naliomba Shirika la ATCL wachape kazi, ndege hizi zimenunuliwa na fedha za Watanzania. Nitoe wito kwa wafanyakazi wa ATCL kuwahudumia wateja wake vizuri na kutoa majibu mazuri kwa abiria, nimesikia kuna muda mna wajibu abiria ndege imejaa wakati kwenye ndege siti bado zipo, mnapaswa kuwaona wateja kama wafalme.
“Hivi karibuni nikiwa Mpanda nilitoa agizo kuanzisha safari ya ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mpanda na nimepewa taarifa kuwa safari zimeanza leo na ndege imekwenda ikiwa imejaa na inarudi ikiwa imejaa,” amesema Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jaffo kumpatia Sh bilioni 1.5 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kama alivyoomba kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo; “ Ukazitafute hizo fedha na umpatie akajenge hospitali ya Wilaya ya Ubungo.”