Ruvuma: Mbaroni Akituhumiwa Kuua Mdogo Wake

JESHI la Polisi linamshikilia Mohamed Luambano (70) mkazi wa Mtelamwai wilayani Namtumbo kwa tuhuma za kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani na kiganja cha mkono wa kulia mdogo wake, Abeid Luambano (65) na hatimaye kufariki dunia.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 2:00 usiku katika kitongoji cha Doroba kilichoko katika kijiji cha Mtelemwai.



Alisema inadaiwa siku ya tukio, Abeid alikutwa akiwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na pia kukatwa kiganja cha mkono wa kulia na watu wasiofahamika.



Maigwa alisema Abeid kabla ya kuuawa, alivamiwa ghafla na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kisha kutolewa nje ya nyumba yake na kuanza kupigwa na kitu chenye ncha kali hadi kupoteza maisha.



Kutokana na tukio hilo, alisema Luambano ambaye ni kaka wa marehemu, amekamatwa kwa mahojiano zaidi kutokana na madai kwamba siku za karibuni kumekuwapo na kutoelewana kati ya ndugu hao.



Alisema ugomvi huo ulisababishwa na Abeid kuchomewa nyumba yake aliyokuwa akiishi akimtuhumu kaka yake na mtoto wake aliyetajwa kwa jina la Msajiri kuwa walikuwa wakimfanyia vitu vibaya.



Mtoto huyo wa Luambano amekimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya tukio hilo la mauaji na  Kamanda Maigwa alisema juhudi za kumtafuta zinaendelea.



Katika tukio lingine, Nuru Milanzi, mfanyabiashara mdogo na mkazi wa Mashujaa, Manispaa ya Songea, amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya manira ndani ya chumba alichokuwa analala.



Kamanda Maigwa alisema tukio lilitokea juzi majira ya saa 1:00 usiku baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mashujaa, kutoa taarifa kituo cha polisi kuwa Milanzi amekutwa nyumbani kwake akiwa amejinyonga na kufariki dunia.



Alisema inadaiwa chanzo cha kujinyonga kwake  ni madeni yaliyokithiri kwenye Vicoba ambayo yalimsababishia msongo wa mawazo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad