Serikali yaagiza wafugaji kuunga mkono uhamilishaji Mifugo
0
October 12, 2019
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka wafugaji kuunga mkono zoezi la uhamilishaji ng’ombe ili kuweza kufikia malengo ya kukidhi mahitaji ya malighafi za Viwanda nchini na kupata maboresho ya koosafu.
Ulega ametoa wito huo jana wakati akizindua kampeni ya uhamilishaji wa ng’ombe uliofanyika katika eneo la kambi ya Ranya, lililopo Ranchi ya Taifa (NARCO), Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Vijana Ruagwa wafurahia mafunzo ya kilimo
Amesema lengo la kufanya uhamishaji huo ni kupata ng’ombe milioni moja kwa mwaka ili kuboresha koosafu kutoka ng’ombe za asili na kuboresha mifugo ikiwa ni lengo la kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli za Tanzania ya Viwanda.
“Tunataka tupate ng’ombe wa kutosha wenye kuweza kuingiza malighafi kwenye viwanda tunavyojenga, hivi sasa tunajenga viwanda vingi vya uchinjaji na uchakataji wa mazao ya mifugo, hivyo vyote vinahitaji malighafi hivyo tunataka mifugo yetu izidi kuzaliana,” ameongeza Ulega.
Aidha Naibu waziri Ulega amefafanua kuwa wamedhamiria kupata ng’ombe wenye uwezo wa kuhimili magonjwa na walio na kilo za kutosha na kwamba ni juhudi za wafugaji kuhakikisha wanaipatia mifugo malisho bora na chanjo.
“Tulishafanya uzinduzi wa kambi la mkoa wa Simiyu na tumepata ng’ombe takribani laki saba kwa leo tunafanya hapa Kongwa lakini ni matarajio yetu pia kufika Mikoa ya Rukwa na Katavi na tuna makisio kati ya asilimia 60 hadi 70 ya kuhakikisha tunapata ndama,” amefafanua Ulega.
Amesema Ng’ombe watakao wapandishwa kwa Ranchi ya kongwa ni 67,000 ambao wameonekana kuwa na uwezo wa kufanyiwa zoezi hilo huku akisema asilimia 60 hadi 70 ya ng’ombe hao wanatarajiwa kupata mimba na kuwataka wafugaji nchini kuunga mkono zoezi hilo la uboreshaji koosafu.
“Katika zoezi hili kila mfugaji atachangia Sh.5,000 kwa ajili ya ng’ombe kuchomwa homoni na tutatumia mbalimbali za upandishaji kwa kutumia mirija kwa maana ya chupa, kutumia viini tete na njia hii itakapokuwa tayari tutaisambaza na tumetoa mbegu hizi bure,” amefafanua zaidi Naibu Waziri wa Mifugo Abdallah Ulega.
Tags