MASHABIKI wa Simba hivi sasa wana jeuri sana. Ukikaa pale klabuni Msimbazi utacheka sana. Jeuri yao imepitiliza hadi kufikia hatua ya kuitaka Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwapangia wacheze mechi mbili kwa siku moja.
Si unafahamu kwamba Jumatano ya wiki ijayo yaani Oktoba 23, mwaka huu wanacheza na Azam FC pale Uwanja wa Uhuru, basi siku hiyohiyo pia wanataka wacheze na Yanga. Wanaona Januari 4, mwakani ni mbali sana.
Wanawataka mapema.
Ukiangalia kwenye Ligi Kuu Bara, Simba ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi nne na kushinda zote.
Wao na Azam ambao wanashika nafasi ya pili, peke yao ndiyo wameshinda mechi zote walizocheza hadi sasa. Azam wamecheza mechi tatu na kushinda zote.
Sasa vikosi hivyo ambavyo wanatamba navyo Simba kwamba vina uwezo wa kucheza mechi viwanja tofauti kwa siku moja na kushinda bila ya wasiwasi ni hivi hapa:
SIMBA VS YANGA
Wenyewe wanasema mchezo huu uchezwe Uwanja wa Taifa jijini Dar. Kikosi ambacho kitacheza dhidi ya Yanga wanataka Aishi Manula akae langoni.
Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa wasimamie ulinzi huku pale kati wakiwapanga Jonas Mkude na Clatous Chama. Mastaa wengine waliowaweka kwenye kikosi hiki ni Mzamiru Yassin, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga.
Katika kikosi hicho, wachezaji wote hao walikuwa Simba msimu uliopita na bado anaendelea kupambana kuhakikisha wanatetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara. Wanaamini kwamba kikosi hicho kinaweza kuisimamisha Yanga bila presha yoyote kwenye Uwanja wa Taifa.
SIMBA VS AZAM
Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar, mashabiki wa Simba wanasema wataenda na kikosi hiki siku hiyohiyo ya Jumatano:
Beno Kakolanya, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Tairone Santos, Gerson
Vieira, Deo Kanda, Sharaf Shiboub, Miraj Athuman, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata. Hapo kuna wengine kibao wako benchi wakiwemo vijana.
Kikosi hiki wanachotamba kwamba kinawatosha Azam, kinajumuisha wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba msimu huu na ambao wanafanya vizuri kila wanapopewa nafasi. Ni mashine ambazo lengo la Kocha na uongozi wa Simba ilikuwa kuwatumia kuongeza nguvu kwenye michuano ya kimataifa ambayo walitolewa mapema bila kutarajia.