Tigo Fiesta Ilivyoacha Historia Dodoma


ZAIDI ya wasanii 16 juzi walitingisha baada ya kutoa burudani ya aina yake katika tamasha la Tigo Fiesta Saizi Yako, lililofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma. Juzi ilikuwa zamu ya Jiji la Dodoma na maeneo jirani kupata burudani hiyo ya aina yake baada ya kufanyika mikoa mingine mitatu tangu tamasha hilo lililopozinduliwa msimu huu.



Katika tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako mjini Dodoma, walihudhuria viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mawaziri na wabunge pamoja na mashabiki kutoka katika kila kona ya mkoa huo.



Kabla ya kuanza tamasha la Tigo Fiesta 2019, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Paul Kunambi, aliwatambulisha baadhi ya wabunge na mawaziri ambao walihudhuria kwenye tamasha hilo.


MKALI wa nyimbo za injili Godluck Gozbert akilishambulia jukwaa la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako katika tamasha lililofanyika juzi Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.



Kunambi alisema kuwa tamasha hilo kwa mwaka huu limetoa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukuza biashara za wajasiriamali kutokana na kuongeza mitaji.



Alisema kuwa kumekuwa na ajira za muda mfupi ambazo zinachangiwa na tamasha hilo ikiwa ni sehemu ya kukuza kipato kwa vijana.



Alisema anaishukuru Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo kutokana na kuonyesha ubunifu wa hali ya juu na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako.




Mwanadada Marianne Mdee ‘Mimi Mars’ akifanya vitu vyake kwenye tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako, lililofanyika juzi Uwanja wa Jamhuru mjini Dodoma.

“Tunaishukuru Tigo kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na ubunifu wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuendeleza vijana kupitia muziki wa bongo fleva,” alisema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo Kanda ya Kaskazini, Idan Komba, alisema wanaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli kwa kuhakikisha wanakamilisha usajili kwa alama za vidole kwa wateja wote wa Tigo nchini.



“Tutaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usajili wa alama za vidole unafanyika na kuwafikia wateja wote wa simu za Tigo nchini,” alisema.

Tamasha hilo lilianza kwa wasanii chipukizi kupanda jukwaani na baadaye alipanda mkali wa bongo fleva anayefanya vizuri kwa sasa, Badest na kuimba kibao chake cha Nikagongee kilichowainua mashabiki na kuanza kumshangilia kwa kupiga kelele.



Baadaye alipanda jukwaani Heri Samir ‘Mr Blue’, na kuonyesha makali yake ikiwa ni pamoja na kuporomosha vibao vya zamani na vile vinavyotamba kwa sasa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.

Mr Blue alianza na wimbo wa Tabasamu ambao aliimba live pamoja na bendi, baadaye akapiga wimbo wa Mbwa Koko, na kumalizia na Mboga Saba iliyowafanya mashabiki kuimba naye mwanzo hadi mwisho wa wimbo huo.



Hata hivyo Mr Blue alionyesha ukomavu wa hali ya juu kwenye onyesho la Tigo Fiesta Saizi Yako baada ya kumpandisha Nurdin Bilal ‘Shetta’, na kushirikiana naye kuimba wimbo wa Hatufanani.

Baadaye Shetta alibaki mwenyewe jukwaani na kutoa burudani kabambe ikiwa ni pamoja na kuimba nyimbo kama Shikorobo ilioonekana kuwavutia sana mashabiki waliohudhuria kwenye tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako.



Msanii wa bongo fleva, Abdul Chande ‘Dogo Janja’alipanda jukwaani na kutoa burudani murua ambapo aliimba nyimbo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ngarenaro, Kilele na Yente.




NYOTA wa muziki wa bongo fleva Heri Samir ‘Mr Blue’ akiimba katika tamasha la Tigo Fiesta 2019.



Nyota wa muziki wa injili, Godluck Gozbert alipewa nafasi kubwa na mashabiki kwenye tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako baada ya kupanda jukwaani na kuimba nyimbo mbalimbali zinazofanya vyema kwa sasa.

Staili aliyoingia nayo msanii huyo ilikuwa ya kipekee na kuwafanya mashabiki kumshangilia kwa kiasi kikubwa baada ya kuimba nyimbo za Shukrani, Nibadilishe na Hauwezi Kushindana. Mwanadada Marianne Mdee ‘Mimi Mars’ alipanda jukwaani na kuonyesha manjonjo akiwa na wanenguaji wake.



Msanii huyo anayefanya vizuri kwenye muziki wa bongo fleva, alitawala vilivyo jukwaa kutokana na kuimba nyimbo zilizoteka hisia za mashabiki wake. Msanii huyo aliimba wimbo wa Kodo, Polepole pamoja na Muwa na kuwafanya mashabiki kumshangilia vilivyo.

Wasanii wengine waliopanda jukwani kwenye tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako, ni pamoja na Barnaba Elias, Marioo, Juma Jux na Weusi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad