Sydney, Australia (AFP). Mchumi wa Australia ambaye alitumia kimakosa takriban miaka ishirini gerezani kutokana na mauaji ya ofisa mwandamizi wa polisi, atafidiwa zaidi ya dola 4.74 milioni (takriban Sh9 bilioni za Kitanzania).
David Eastman, mtumishi wa zamani wa serikali, alipatikana na hatia ya kumuua ofisa huyo wa polisi, Colin Winchester mwaka 1995 na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Eastman, ambaye mara zote amekuwa akisisitiza kuwa hakuhusika na mauaji hayo na kufanya majaribio kadhaa ya kukata rufaa, aliachiwa huru mwaka 2014 baada ya hukumu yake kubatilishwa.
Mahakama ya Juu ya Australia (ACT) ilifanya uamuzi huo wa serikali kumlipa Eastman Sh9 bilioni za fidia.
Eastman alikuwa akidai fidia ya angalau Sh40 bilioni.
Eastman mwenye umri wa miaka 74 aliiambia mahakama kuwa alipoteza fursa si tu ya kuwa na familia na kuendeleza kazi yake, bali pia mama na dada zake walifariki wakati akiwa gerezani.
Mahakama pia iliambiwa kuwa alishuhudia mauaji wakati akiwa katika kituo cha mahabusu na bado anasumbuliwa na uonaji hafifu wa jicho moja baada ya kushambuliwa na mfungwa mwingine.
Mwanasheria Sam Tierney aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama mjini Canberra kuwa mteja wake hajafurahia uamuzi huo.
"Alipoteza kitu kikubwa katika maisha yake na sasa atakuwa na mawazo kichwani kwake kwamba atafanyia nini fedha hizo," alisema.
Haikuweza kueleweka kama Serikali itakata rufaa kupinga uamuzi huo. Keshi hiyo imeshaigharimu serikali fedha nyingi.
Winchester alipigwa risasi wakati akitoka kwenye gari karibu na nyumbani kwake katika kitongoji nje ya Canberra mwaka 1989.