Uganda Kubadili Sheria, Wapenzi wa Jinsia Moja Kunyongwa


Kampala. Waziri wa Maadili nchini Uganda, Simon Lokodo ametangaza mipango wa kuanzisha tena sheria inayopinga mahusiano ya jinsia moja iliyofutwa na mahakama ya kikatiba mwaka 2014.

Waziri huyo ameliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, kuwa sheria hiyo mpya itatoa hukumu ya kifo kwa yeyote atakayetiwa hatiani kwa makosa hayo.

“Sheria yetu ya sasa inatubana sana. Inasema kuwa kitendo hiki ni jambo la kuvunja sheria. Tunataka iwekwe wazi kuwa mtu yeyote anayepigia debe suala hili anaweza kushtakiwa. Wale wanaofanya vitendo vya kushangaza watahukumiwa kifo,” alisema

Aliendelea kueleza kuwa, “mahusiano ya aina hii si kitu cha kawaida kwa watu wa Uganda na kumekuwa na waajiriwa wengi shuleni ambao ni wapenzi wa jinsia moja wanaowafundisha watu uongo kuwa mtu anazaliwa na hisia za mapenzi ya jinsia moja.”

Februari 2014, Rais Yoweri Museveni alisaini muswada wa sheria wa kuwabana wapenzi wa jinsia moja lakini sheria hiyo ilifutwa na mahakama Agosti mwaka huohuo.

Mabadiliko hayo yalitokea baada ya kubainika kuwa wabunge walipitisha sheria hiyo bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Lokodo amesema muswada mpya ambao utawasilishwa bungeni wiki zijazo, unaungwa mkono na wabunge na Rais Museveni.

Miaka mitano iliyopita nchi za Afrika Mashariki ziliweka vikwazo na Marekani kwenye uombaji wa viza na wakasitisha utoaji msaada na mazoezi ya kijeshi.

Lokodo amesema nchi yake ipo tayari kwa mashambulio yoyote watakayoyapata juu ya kampeni hiyo.

“Hatupendi kutumiwa. Hatuwezi kusikiliza watu ambao wanataka tukubali suala ambalo ni kinyume na maadili yetu,’’ alisema.

Kwa sheria za sasa hivi ambazo ni za kutoka enzi za ukoloni wa Waingereza, mapenzi ya jinsia moja ni kosa ambalo watu wanaweza kupewa adhabu ya kifungo cha maisha na wanaharakati wanasema sheria hii mpya itaanzisha mashambulizi makali kwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad