Mwanza. Rais John Magufuli ameshasema hana mpango wa kuendelea kukaa madarakani baada ya muda wake kuisha, lakini hiyo haijatosha kuzuia mjadala kuhusu kuongeza muda wa urais, na sasa kuondoa kabisa ukomo.
Kuanzia wakati mbunge wa Nchemba, Juma Nkamia alipotaka kuwasilisha hoja binafsi ya kuongeza muda wa urais kutoka miaka mitano kwenda miaka saba, hadi Desdellius Patrick Mgoya kuhoji tafsiri ya ibara inayomzuia mtu aliyeshika urais kwa vipindi viwili kugombea tena, mjadala huo sasa unakua taratibu.
Hapo katikati mjadala huo ulikuwa ukiibuka na kuzimika na kuibuka tena, lakini umeanza kushika kasi baada ya Mgoya kufungua kesi hiyo ya kuhoji ukomo wa urais.
Wakizungumzia kuibuka na kuzimika kwa mjadala huo, wachambuzi wamesema huenda suala hilo likafikia hatua ya kubadili Katiba, wengine wakisema ni haki ya kikatiba watu kutoa maoni yao na wengine wakisema ni hofu ya baadhi ya watu kupoteza madaraka.
“Watu wana maono yao, watu wana matakwa yao,” alisema Kanali Ngemela Lubinga, katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM.
“Wakati (Rais wa kwanza, Julius) Nyerere anataka kung’atuka walihoji wakisema nchi itakwisha. Waliona ujenzi wa ujamaa hautaendelea, lakini Mwalimu aliwajibu akisema hao ndio maadui wa ujamaa.