Kikubwa ninachowasikia wakiongea ni juu ya ngoma mpya iliyoachiwa na aliyekuwa memba mwenzao kabla ya kuota mbawa, Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize au Harmo iitwayo Uno.
Sitaki nikusimulie, lakini shuhudia mwenyewe wanachokiongea watu hawa hapa mjengoni.
BABU: Ngoja niongee kama mmoja wa kiongozi, kabla hatujaingia kwenye hili lililotuleta hapa, mmesikia mahojiano yake vizuri?
MALKIA: Tumesikia sana, ila ametukosea sana!
MAKOPA KOPA: Malkia kuwa mpole.
BABU: Sasa amesema kwamba tumemfanya ameuza nyumba zake tatu ili kuvunja mkataba wake wa milioni mia tano. Hivi Saidi yana ukweli haya?
SAIDI: Kimsingi tuache hilo, tujadili lililotuleta.
BABU: Hapana Saidi, vitu vingine lazima mashabiki wajue ukweli.
Saidi: Babu, tafadhali twende kwenye pointi tuendelee na majukumu mengine. (Wote wanapiga makofi kuonesha wamekubaliana na maneno ya Saidi).
BABU: Wangapi wamesikia Uno?
MAKOPA KOPA: Tumesikia, lakini noma yenyewe mbayaaa!
DHAHABU: Duh! Nilijipanga vya kutosha nikiamini litakuwa dude balaa, sijaamini kumbe wa kawaida sana!
MALKIA: (anacheka).
BABU: Mimi binafsi nimeona ni bonge la ngoma na ndilo lililofanya tukutane hapa. Angalia hadi leo lipo kwenye trending namba moja huko YouTube. Mwanzoni alisema ataachia muda wa usikuusiku hivi kesho yake tukaleta uzinduzi wa kipindi cha michezo kumzima, lakini hii ya sasa ameachia kimyakimya.
MABOSSI: Unajua bosi alichokifanya ni nini? Amesubiri Dhahabu ameenda Canada kwenye shoo na Roy ndiyo akaachia. Angesubiri angeona hizo fitna.
BABU: Sasa tujipange, tunamkabili vipi kumzima?
DHAHABU: Si umeona nilichokifanya mimi, nimeingia Twitter yangu nikamfagilia kinoma ili kuwateka mashabiki alioondoka nao watuone bado tuna uhusiano naye.
BABU: Nimeona ni jambo zuri sana umefanya. Kingine nimeona kwenye kava lake la Uno bado katutendea haki kuiweka logo ya WCB. Asingeweka tungemfungia nyimbo zake zote alizofanya kwetu asizicheze popote.
Mkakati mwingine wa kufanya, Dhahabu kama inawezekana na wewe kufanya mahojiano exclusive kabisa na TV au radio yoyote isiwe ya kwetu hapa. Ukamuelezea kwa mazuri tu, ukifanya hivi watu watakuongelea wewe na kuuzima wimbo wake.
DHAHABU: Babu una akili nyingi sana, ndiyo maana nakukubali.
Malkia: Lakini mmeona njia anazopita? Anafanya listening party za uzinduzi wa wimbo wake kila baa, nimeona anafanya hivyo hadi Kenya na Uganda huko, hapo tutamzimaje sasa kwa vyombo vya huko watakavyokuwa wanampaisha?
SAIDI: Malkia mdogo wangu. Sisi tupo kwenye gemu kwa muda mrefu sana. Hilo jambo dogo sana kwetu kwa kuwa tuna koneksheni kubwa sana.
DHAHABU: Ila inaniuma ile idea ya Uno! Halafu mbaya zaidi anajifanya kunilipizia kwenye wimbo wake kunitaja na mama watoto wangu, kisa nilimuimba kwenye ule wimbo niliofanya na Fally Ipupa.
MAKOPA KOPA: Achana na hilo bro, kuna hili la kumchukua Meninah na kumchezesha kwenye ule uzinduzi wake! Yaani ametumia bonge la akili, si unaona inavyokiki huko mitandaoni?
BABU: Makopa Kopa mdogo wangu! Huyo Harmo amekuja kwetu akiwa hajui lolote. Njia zote anazopitia amezitoa hapa, hilo analofanya dogo tu kwetu!
SAIDI: Lakini Babu, hapo video bado hajaachia anatutikisa hivi mara naona vitisheti vyao, akiingia studio na rundo la watu wakiwa hadi na makopo ya kuwekea maji.
MAKOPA KOPA: Haaa..haaaaa…bosi Saidi siyo makopo yale ni vikombe maalum vya kuwekea maji au juisi. Tena tukifanya na sisi aina hii kwenye mahojiano yetu itakuwa poa sana.
MALKIA: Mimi naona tukiendelea na kikao hiki na watu wakatushtukia, nahisi kama tunampa kiki tu. Kikubwa hapa tuangalie kitu gani cha kuzima hapa kabla hajaachia video.
MAKOPA KOPA: Siyo video hiyo ya Uno tu, bado ataachia video mbili si mmesikia na wimbo wake mwingine wa Niteke Remix akiwa na Maua Sama?
DHAHABU: Dogo naona umeanza wenge na wewe! Angekuwa na dairekta wetu au kutoka Nigeria, Sauz au Marekani sawa, lakini hao sijui kina nani tu wa mtaani. Kwanza mmeshanitibua acha niondoke zangu.
BABU: Dhahabu, Dhahabu acha jazba…
SAIDI: Nini tena unafanya Dhahabu, mtoto mdogo tu huyu hawezi kutusumbua akili zetu.
Naona kila dalili ya kikao hiki kuvunjika kwani hata Makopa Kopa, Malkia na Mabossi wote wameinuka wanaongozana na Dhahabu kusepa. Saidi naye anabaki kwa muda na Babu kama kuna kitu wananong’o-nezana kwa muda kisha nao wanaondoka na kuniacha peke yangu kwenye ukumbi huu!
Loading...
TOA COMMENT