Sanders alikuwa mfanyabiashara wa Marekani na mmiliki wa migahawa iitwayo Kentucky Fried Chicken KFC inayouza vyakula mahususi ikiwamo kuku na chips. Hivyo na wewe hata kama umri umekutupa mkono,usikate tamaa,bado una nafasi ya kutoboa na kuwa tajiri kama Sanders.
Kwa ujumla huyu ndiye mwanzilishi wa migahawa maarufu ya KFC duniani.Licha ya kustaafu kazi akiwa ‘fukara wa kutupwa’katika umri wa miaka 65,lakini hadi anafariki mwaka 1980 akiwa na umri wa miaka 90,alikuwa kwenye orodha ya mabilionea wakubwa wa Marekani.
Kwasasa migahawa ya KFC imeenea katika nchi 123 duniani, hata Tanzania pia imo.Ni migahawa ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya McDonald’s kwa kuuza misosi inayopendwa na wengi.Mwaka 2013, migahawa ya KFC ilifanya mauzo ya dola bilioni 23 (zaidi ya Shilingi trilioni 50).
HISTORIA
Kama ilivyo kwa baadhi ya mabilionea , Sanders alizaliwa katika familia ya kimaskini.Baba yake, Wilbur David, alikuwa mkulima. Baadaye alivunjika mguu, akahamia kwenye kazi ya kuuza nyama buchani. Mama yake, Margaret Ann alikuwa ni mama wa nyumbani.
Mwaka 1895, Sanders, akiwa na umri wa miaka mitano alipata pigo la kufiwa na baba yake mzazi, David. Siku aliyokufa baba yake alirejea nyumbani kutoka kazini akiwa na homa kali. Hawakuwa na pesa ya kumpeleka hospitalini hivyo ulipofika usiku alifariki dunia kwa kukosa tiba.
Sanders alianza kuhangaika na maisha tangu akiwa na umri mdogo.Haikuchukua muda mrefu tangu baba yake afariki dunia mama yake aliolewa tena na tajiri aliyeitwa William Broaddus.Hata hivyo kibopa huyo huyo hakumpenda Sanders hivyo siku moja alimfukuza nyumbani kwake.
MISUKOSUKO
Safari yake ngumu ya kimaisha ilianza akiwa na umri wa miaka 17 alipoamua kuachana na kazi ya ukulima. Alipata , kazi shirika la reli lililoitwa Norfolk.Huko alikutana na mfanyakazi mwenzake, Josephine na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi.
Sanders na Josephine, walibahatika kupata watoto wawili, Margaret na Mildred.Ugumu wa maisha uliendelea baada ya kufukuzwa kazi kwenye shirika hilo la reli.Baada ya hapo alijiunga na jeshi lakini huko nako alifukuzwa.Baadaye aliajiriwa kwenye kampuni ya Michellin. Huko alikuwa akiuza matairi lakini napo hakudumu kwasababu kampuni hiyo ilifilisika.
Maisha yakaendelea, akaajiriwa kwenye shirika la bima ambako napo alifukuzwa.Baadaye alipata tena kazi kwenye kampuni ya kuuza mafuta ya Shell. Hata hivyo kibarua kiliota nyasi baada ya kampuni hiyo nayo kufilisika.Katika hali kama hiyo mkewe alishindwa kuvumlia hivyo aliachana naye huku akiondoka na watoto, akaenda kuishi nao kwa wazazi wake.
KUOSHA VYOMBO
Ugumu wa maisha ulimfanya Sanders kuajiriwa na kazi yake safari hii ilikuwa kuosha vyombo mgahawani. Huko alijifunza kupika vyakula mbalimbali.Hata hivyo umri nao ulikuwa umemtupa mkono hivyo alilazimika kustaafu akiwa na umri wa miaka 65.
KUJIUA
Baada ya kustaafu, Sanders alikutana na mfanyabiashara Peter Harman, akampa wazo la kuanzisha mgahawa Kentucky Fried Chicken, biashara yao kubwa ilikuwa kuuza nyama ya kuku. Biashara ya kuku ilikuwa maarufu kwani walifungua matawi mengi.
Wakati Sanders anastafu mafao yake yalikuwa kiduchu kiasi cha dola 105.(takribani 200,000 na ushee).Kiasi kilichomuumiza hivyo akataka kujiua.Aliona hakuna thamani ya kuishi tena,lakini alipojifikiria mara mbili, alisitisha jaribio lake hilo.
APATA FIKIRA MPYA
Alichokifanya Sanders ni kukaa chini ya mti akaandika matarajio yake.Katika kutafakari, aligundua jambo moja ambalo anaweza kulifanya vizuri zaidi kuliko mtu yoyote.Kwa kutumia jina Kentucky Fried Chicken, alichukua dola 87 kama(takribani Shilingi 200,000)kutoka kwenye mafao yake na kununua kuku. Akawakaanga kwa mchanganyiko wa viungo mbalimbali,akapata mchanganyiko unaovutia na wenye ladha ya kipekee.
Alikuwa akipita mlango kwa mlango kuwauza kwa majirani zake huko Kentucky na mwishowe akajikuta akianzisha migahawa na kufungua matawi kwenye miji mbalimbali na taratibu akaanza kuona mafanikio.
Hatimaye biashara yake ikakua na akafungua migahawa mingi ya KFC nchini Marekani. Mchanganyiko ule ukazidi kupendwa na kutanua wigo ya biashara yake na kujikuta akiogelea kwenye bwawa la utajiri kabla ya kifo chake.
SOMO KWA ANAYETAKAA UTAJIRI
Sanders anatoa somo yeye alikuwa fukara hadi uzeeni na kudhani alishindwa maisha na kutaka kujiua.Lakini, baada ya kutafakari na kujaribu hatimaye Mungu akamfanikisha. Jiulize umekata tamaa ya maisha? Ulitamani kusoma lakini ukashindwa kwa kukosa ada? Umesoma japo huna ajira? Miaka inapita na unaona wenzio wanaajiriwa wewe uko nyumbani? Je,umejaribu biashara lakini kila wakati unapata hasara? Unahisi kukata tamaa? Unaanza kuwaza Mungu amekuacha? Usikate tamaa, Mungu yupo pamoja na wewe, jipange na jifunze kutoka kwa wakali kama Sanders.