Vita ya Wasafi Vs Konde… Rayvanny Amfanyia Umafia Harmo


NI wazi sasa kwamba kitendo cha mkali wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kujitoa kwenye lebo iliyomlea ya Wasafi Classic Baby (WCB), kimezaa uhasama mkubwa kati yake na lebo yake Konde Music Worldwide na wanamuziki wa lebo hiyo, Risasi Mchanganyiko limedokezwa.



Imeelezwa kuwa, vita ya Wasafi dhidi ya Konde Music sasa ni piga nikupige. Mmoja wa wanamuziki wa Lebo ya Wasafi iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, anadaiwa kumfanyia umafia Harmonize au Harmo.



KISA KAMILI

Risasi Mchanganyiko linafahamu kwamba, Ijumaa iliyopita Harmo alikuwa aachie wimbo wake mpya wa Uno na kuibua gumzo kubwa kwa mashabiki waliokuwa wakiusubiria kwa shauku.

Hata hivyo, katika mazingira ya sintofahamu, muda ule wa jioni aliosema ataachia wimbo huo, watu wakapigwa na butwaa kuona ghafla Rayvanny akiachia wimbo wake wa Slow.

YUPO NA PHYNO WA NIGERIA

Ndani ya wimbo huo, Rayvanny amemshirikisha mwanamuziki mwingine mkubwa wa Nigeria, Rapa Phyno ambaye mapema mwezi uliopita aliachia wimbo wake wa Baby akiwa na Harmo.

KUHUSU WIMBO WA HARMO

Gazeti hili linafahamu kwamba, imepita miezi kadhaa bila Harmo kuachia ngoma yake mpya zaidi ya kushirikishwa au kushirikiana na wanamuziki wa nje ya Bongo na hasa baada ya kusepa Wasafi. Hicho ndicho kilichosababisha mashabiki wake wengi standby (kusubiria) ujio wa Harmo.

Tangazo la Harmo kupitia ukurasa wake wa Instagram lilipata maoni mengi huku kila mmoja akiwa na shauku ya kusikia na kuona ngoma hiyo ya Uno. Wakati mashabiki wakisubiria ujio huo ndipo Rayvanny alipotawala ghafla kwenye mitandao ya kijamii akiwa na wimbo wake huo mpya, hivyo akawa amemzima Harmo.

Imeelezwa kuwa kwa sasa lebo hizo mbili zinafanyiana umafia kwani baada ya Wasafi kusikia Harmo anaachia wimbo mpya ndipo wakaachia huo wa Rayvanny ili kuuzima wa Harmo kwani timu ya Wasafi ilianza kuusambaza na kuusifia hivyo kuwa ndiyo habari ya mjini.

Kwa upande wake, Harmo aliona ili kuzikwepa hujuma hizo ni bora akae kimya kwanza na sasa ngoma hiyo itabidi aiachie ghafla bila matangazo ili kukwepa hujuma.

YATOKANAYO…

Habari kutoka kwenye vyanzo vyetu vya kuaminika zinaeleza kuwa, tangu kuondoka kwa Harmo kwenye Lebo ya Wasafi, kumekuwa na harakati za ndani zinazofanywa kumpaisha memba mwingine wa kundi hilo ambaye ni Rayvanny ili kuziba pengo la Harmo.

Habari za chini ya kapeti zinaeleza kuwa, mwaka huu wa 2019 huenda ukamalizika kwa mafanikio makubwa kwa Rayvanny kutokana na ‘fujo’ zinazofanyika za kumpaisha kimataifa.

Imedaiwa kuwa, kasi yake ya kufanya kolabo za kimataifa ni kubwa kama aliyokuwa nayo Harmo alipokuwa ndani ya lebo hiyo. Mpaka sasa Rayvanny ameshafanya kolabo na wanamuziki wakubwa duniani kama Pitbull, Jason Derulo, Nora Fatehi na sasa Phyno.

Habari nyingine nzito ni kwamba kwa sasa Rayvanny yupo kwenye maandalizi ya kolabo na mwanamuziki aliyewahi kufanya kazi chini ya lebo ya rapa mkubwa duniani, Jay-Z kupitia lebo yake ya Roc Nation anayefahamika kwa jina la Philly Freeway.

Kwa mujibu wa prodyuza maarufu wa Bongo Fleva, S2kizzy, Rayvanny na jamaa huyo tayari wameingia studio nchini Marekani na mwanamuziki mwingine anayefanya vizuri nchini Netherlands aitwaye Frenna.

UZINDUZI MGAHAWA, VIPINDI WASAFI

Jumapili iliyopita Harmo alizindua mgahawa wa ugawaji wa chakula bure jijini Dar wa Konde Boy. Wachunguzi wa mambo walidai kuwa, Harmo alifanya hivyo ili kuzima tukio la Wasafi la uzinduzi wa vipindi vyao vya redio na runinga.

Baada ya ugawaji wa chakula bure kuliibuka ‘vurugu’ za kutosha mtandaoni ambapo Harmo alipokea sifa kama zote kwa tukio hilo la kurudisha kwa jamii. Hata hivyo, kulipokucha pongezi zilikata na kuhamia kwa Diamond na Wasafi yake kutokana na uzinduzi baab’kubwa wa vipindi vyao vya redio na runinga.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad