Watoto wa Bilionea Msuya Hali Bado Tete
0
October 20, 2019
Arusha. Licha ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro kuagiza watoto wa marehemu bilionea Erasto Msuya kurejea katika makazi ya baba yao yaliyopo eneo la Sakina jijini hapa, imeshindikana.
Akizungumza jana na Mwananchi mtoto mkubwa wa Msuya, Kelvin Msuya (22) alisema wameshindwa kurejea katika makazi yao kutokana na kutokamilika kwa masuala ya kisheria.
Kelvin alisema hiyo imetokana baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo na kubainika nyumba hiyo ni sehemu ya mali ambazo zimeandikwa na bibi yake, Ndeshekuru Sikawa katika kesi ya mirathi.
“Leo (jana) tangu asubuhi tuliitwa polisi kutoa maelezo ya mgogoro huu, sasa inavyoonekana kuna masuala ya kisheria bado Serikali inafanya ili kuhakikisha tunapata haki yetu,” alisema.
Kelvin alisema wito huo wa polisi ulitokana na maagizo ya mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye pia alitaka suala hilo kushughulikiwa na kumalizwa kwa amani na utulivu.
“Hivyo nimeona kwa kuwa Jumatatu tuna kikao na ndugu wa baba tunaweza kukamilisha baadhi ya mambo ili hata nikirejea katika makazi niishi kwa amani,” alisema Kelvin.
Alisema sasa yupo peke yake nchini, wadogo zake wawili bado wapo shule Nairobi nchini Kenya.
Hata hivyo, Kelvin aliomba Serikali kusaidia kesi ambayo inamkabili mama yake, kusikilizwa kwani ndugu hao wa baba yake wamekuwa wakiweka mapingamizi ambayo yanalenga kucheleweshwa kesi.
Muro juzi baada ya kueleza kupata mgogoro huo kupitia vyombo vya habari, aliamua kuzikutanisha pande zote zinazogombania mali za bilionea huyo wakiwapo wazazi wake.
Nyumba hiyo waliorejeshewa watoto kuishi ni kati ya nyumba tano zilizokuwa zimefungwa na ndugu wa bilionea huyo, kwa kile walichoeleza sababu za kiusalama na zipo katika kesi mpya ya kuomba usimamizi wa mirathi iliyofunguliwa na mama wa Msuya, Ndeshukuru Sikawa.
Muro alisema sambamba na kuwarejesha watoto katika nyumba hiyo, aliwataka wawakilishi wa familia ya Msuya na mke wake, Miriam Mrita kukutana ofisini kwake Jumatatu kuzungumzia mwafaka wa mgogoro huo.
Miriam anashikiliwa gereza la Segerea kwa tuhuma za mauaji ya dada wa bilionea huyu, Aneth.
Hata hivyo, dada wa bilionea huyo, Upendo Msuya alisema wanafamilia hawana nia ya kudhulumu mali ya watoto bali walifunga nyumba kwa sababu za usalama baada ya kuona ndugu wa mke wa wakichukuwa vitu.
Mwananchi
Tags