Watumishi wa Ardhi ‘waliokacha’ Mafia kikaangoni


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameagiza kupatiwa majina ya watumishi saba wa sekta ya ardhi waliopangiwa kuhamia halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani lakini hawajaripoti katika vituo vyao vya kazi.

Dkt. Mabula ametoa agizo hilo jana alipo anza ziara yake ya siku mbili katika wilaya ya Mafia mkoani Pwani, kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki, kukagua Masijala ya ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi.

Agizo hilo amelitoa baada ya kuelezwa na Mkuu wa wilaya ya Mafia, Shaib Nnunduma kuwa wilaya yake ina mtumishi mmoja wa sekta ya aridhi jambo linaloifanya wilaya hiyo kushindwa kutekeleza majukumu ya sekta hiyo ipasavyo.

Mabula amesema, wizara yake italifanyia kazi suala hilo mapema kwa kuwa ni vigumu wilaya kufanya kazi vizuri katika sekta ya ardhi kwa kutegemea mtumishi mmoja hasa ikizingatiwa sekta hiyo inahitaji kuwa na wapimaji, wathamini pamoja na wataalamu wa mipango miji.

‘’Mafia mna mtumishi mmoja wa sekta ya ardhi? Suala hili inabidi lifanyiwe kazi mapema na wizara yangu italifanyia kazi kuhakikisha wilaya inakuwa na watumishi wa nyanja zote katika sekta ya ardhi’’ amesema Dkt Mabula

Mkuu wa wilaya ya Mafia, Nnunduma alimueleza naibu waziri kuwa, changamoto kubwa inayoikabili wilaya yake kwa upande wa sekta ya ardhi ni kukosekana watumishi wa kutosha ambapo wilaya hiyo imekuwa na mtumishi mmoja wa sekta hiyo kwa muda mrefu baada ya mtumishi mmoja wa Uthamini kupangiwa majukumu mengine.

Kwa mujibu wa Nnunduma, jitihada za wilaya yake kufuatilia upatikanaji watumishi wa sekta ya ardhi zimeonekana kukwama kwa kuwa hadi sasa hawajapata mtumishi mwingine jambo linaloifanya wilaya hiyo kushindwa kutekeleza vyema majukumu ya sekta hiyo.

‘’Watumishi saba walipangiwa kuja Mafia lakini wameshindwa kuripoti na hapa unavyotuona tuna mtumishi mmoja, hatuna wataalamu kama wangekuwepo wangesaidia upangaji. wilaya ni kama imesimama katika sekta ya ardhi’’ alisema Nnunduma.

Mbunge wa jimbo la Mafia Mbaraka Dau, alimueleza dkt Mabula kuwa, pamoja na changamoto nyingine lakini wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa Baraza la ardhi la nyumba  la wilaya jambo linalowalazimu wananchi kufunga safari hadi katika Baraza la Mkuranga kitu alichokieleza kinawafanya baadhi ya wananchi kushindwa kwenda na hivyo kupoteza haki zao
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad