Watumishi watahadharishwa kugeuka Adui namba moja kwa serikali

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuzingatia suala la nidhamu, uadilifu na ubora wa utendaji wao wa kazi ili kuweza kuwahudumia wananchi kiufasaha.

Waziri Hasunga ametoa wito huo jijini Dodoma Oktoba 30, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo alipotembelea ofisi hizo zilizopo eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Amesema udilifu, nidhamu na weledi kwa watumishi wa umma ni kinga dhidi ya
matumizi mabaya ya ofisi za umma na ni moja kati ya njia zinazowawezesha watumishi kufanya kazi kwa bidii.


“Ubora wa kazi zetu na utendaji wa kazi unaozingatia weledi vitaweza kufikiwa kwa kuajiri watumishi wenye sifa stahiki, maadili, na bidii kazini na ambao wanaoweza kwenda na kasi ya mageuzi ya wizara ya kilimo,” amefafanua Hasunga.

Aidha amebainisha kuwa utendaji mzuri wa majukumu ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020.

Kufuatia hatua hiyo Waziri Hasunga amewataka watumishi hao kusimama imara katika kufanya kazi na kutumia weledi wao kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kwamba uadilifu ndiyo silaha muhimu katika kufanya kazi ya umma.

“Mtumishi atakayetumia vibaya rasilimali za serikali atahesabika adui namba moja kwa Serikali na eneo analofanyia kazi na zaidi mtumishi wa aina hiyo ataachishwa kazi na si kuhamishwa,” ameongeza Hasunga.

Ziara hiyo ya waziri wa Kilimo ya kukutana na watumishi hao mbali na mambo mengine pia imelenga kusikiliza changamoto zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad