Waziri Biteko Akutana Na Wawekezaji Kujadili Changamoto Za Makaa Ya Mawe


Waziri wa Madini Doto Biteko amewatoa wasiwasi Wawekezaji wa Viwanda vinavyotumia Makaa ya Mawe na kuieleza Kampuni inayochimba Makaa ya Mawe ya TANCOAL kuwa hairuhusiwi kuongeza bei kiholela badala yake inatakiwa kuuza kulingana na bei elekezi iliyopangwa na serikali.

Kauli hiyo ilitolewa Septemba 15, 2019 na Waziri Biteko baada ya kukutana na wawekezaji wa Viwanda vya Saruji na Vigae kujadili changamoto za Makaa ya Mawe katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza.

Katika Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Biteko, kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa huduma za Leseni wa Tume ya Madini Mhandisi, Yahaya Samamba, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mwanza Fredy Mahobe, Afisa Kodi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Venance Kasiki pamoja na wawekezaji wa viwanda vya Tanga Cement, Kada (T) Ceramics Company pamoja na Lake Cement Ltd.

Kampuni hizo tatu za Tanga Cement, Kada (T) Ceramics Company pamoja na Lake Cement Ltd. zinatumia kiasi kikubwa cha Makaa ya Mawe kwa matumizi ya kuyeyushia Mawe kwa ajili ya uzalishaji wa saruji na vigae ambapo zaidi ya nyuzi joto 2000 zinatakiwa ili kuyeyusha Mawe hayo ziliomba kukutana na Waziri wa Madini ili kueleza changamoto zao.

Hatua hiyo ilikuja kutokana na wanunuzi wakubwa wa makaa yam awe nchini kuwa na mvutano wa bei ya Makaa ya Mawe kati yao na mzalishaji wa Makaa hayo kampuni ya TANCOAL anayozalisha Mawe hayo katika eneo la Kitai Mkoani Ruvuma katika Mgodi wa Ngaka.

Mvutano huo ulianza mara baada Serikali kupitia Tume ya Madini Kuitaka Kampuni ya TANCOAL Kulipa deni lake la kiasi cha shilingi Bilioni 23.9 ambazo zilitokana na malimbikizo ya kutolipa mrabaha wa mauzo na usafirishaji wa Makaa hayo pamoja na adhabu ya asilimia 50 kuanzia Septemba 2011 mpaka Juni 2019.

Aidha, Waziri Biteko amezitaka kampuni hizo kuendelea na uzalishaji wa Saruji na Vigae bila kuhofia kupandishiwa bei kwa maana bei hazitapanda kiholela, ameeleza kuwa, Makaa ya Mawe kote nchi yatauzwa kulingana na bei iliyo elekezwa na serikali.

Imeonekana kwamba, deni la kampuni ya TANCOAL kuwa kubwa, kampuni hiyo imeonesha nia ya kupandisha bei kwanye Makaa ya Mawe ili kufidia deni wanalodaiwa na Serikali.

Kwa upande wake, Mdhibiti wa Fedha wa Tanga Cement, Issac Lupokela alimweleza Waziri Biteko kuwa, kitendo cha kupandishiwa bei na kampuni ya TANCOAL ni kama wanawaadhibu kutokana na ukweli kwamba hakuna mbadala wa kununua kwa wingi sehemu ingine makaa hayo baada ya serikali kusitisha uingizwaji wa Makaa ya Mawe nchini.

“Kipindi cha Nyuma tulikuwa tunanunua Makaa ya Mawe kutoka Afrika ya Kusini kwa kuwa Makaa yaliyokuwa yanazalishwa nchini hayakuwa na kiwango cha kutosha hivyo baada ya serikali kusitisha uingizwaji wa Makaa ya Mawe nchini, tulilazimika kushirikiana na kampuni ya TANCOAL ili kutoa elimu ya namna bora ya uzalishaji wa Makaa hayo, leo tunashangaa wameamua kutupandishia bei,” alisema Lupokela.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad