Yanga Chukueni Tahadhari Mapema Kwa Pyramids


NADHANI kila mmoja anafahamu hivi sasa wawakilishi wetu pekee kwenye michuano ya kimataifa ngazi ya klabu, Yanga imepangwa na timu gani.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kupanga ratiba ya michuano hiyo juzi Jumatano.

Yanga ambayo imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa itacheza na Pyramids FC ya Misri. Timu hiyo ni ngeni katika michuano ya kimataifa, lakini ukiifuatilia kwa kina utabaini kwamba ni timu ambayo ina uwekezaji mkubwa na ni tishio katika soka la Misri.

Katika msimamo wa ligi yao, inashika nafasi ya pili msimu huu kitu ambacho Yanga wanatakiwa kwenda kwa uangalifu wa hali ya juu.Mchezo wa kwanza unatarajiwa kuchezwa Oktoba 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam, kisha Novemba 3, mwaka huu, timu hizo zitarudiana huko nchini Misri. Mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kuanzia leo hadi siku ya mchezo wa kwanza siyo mbali, hivyo Yanga inatakiwa kujipanga kisawasawa kuhakikisha inafanya vema kwanza katika mchezo wa nyumbani, kisha marudiano mambo yawe rahisi.

Yanga ambayo naweza kusema ina bahati katika michuano ya Caf msimu huu tangu ilipokuwa Ligi ya Mabingwa Afrika, safari hii inapaswa kuutumia vema uwanja wa nyumbani.


Nikukumbushe tu kuwa, tangu hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ilianzia nyumbani kwa kucheza dhidi ya Township Rollers ya Botswana. Matokeo yalikuwa 1-1, kisha marudiano nchini Botswana Yanga ikashinda 1-0.

Katika hatua ya pili, Yanga ikacheza dhidi ya Zesco United ya Zambia. Mechi ya kwanza ilichezwa hapa nyumbani matokeo yakiwa 1-1, ziliporudiana nchini Zambia, Yanga ikafungwa 2-1. Ikaondoshwa kwenye michuano hiyo na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ipo hivi sasa. Hii ni karata ya mwisho kwa Yanga katika kuhakikisha inaendelea kuibeba Bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa msimu huu baada ya kushuhudiwa timu tatu kuondoshwa mashindanoni.

Tulianza msimu tukiwa na timu nne. Yanga na Simba zilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na KMC zikiwa Kombe la Shirikisho Afrika. Wawakilishi wetu wote hao wameondoshwa kwenye michuano waliyoshiriki msimu huu, kwa bahati nzuri Yanga imeangukia Shirikisho, sehemu ambayo inapaswa kwao kujipanga kwelikweli kusonga mbele.

Benchi la Ufundi la Yanga chini ya Kocha Mwinyi Zahera, linapaswa kuwasoma haraka wapinzani wao ili kutambua mapema ni mbinu gani huwa wanazitumia katika kufanya vizuri kwani timu hiyo hadi inafika hapo, imefanya makubwa sana. Yanga imekuwa na rekodi mbaya inapokutana na timu kutoka Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, safari hii inakwenda tena kukutana na timu kutoka ukanda huo, hivyo Zahera anapaswa kulitambua hilo na kuhakikisha Waarabu hawa wanakufa tena ikiwezekana nje ndani.


Watanzania wengi naamini tupo nyuma ya wawakilishi wetu hawa ambao ndiyo wamebaki pekee kuipeperusha bendera ya nchi hii, tuendelee kuwasapoti kufikia malengo. Kuwasapoti pekee haitoshi, Yanga nayo inapaswa kubadilika kwani ukifuatilia mechi zake zote za kimataifa msimu huu, imefika hapo kwa bahati kubwa.

Imeweza kucheza mechi nne, imefunga mabao matatu na kufungwa manne. Si rekodi nzuri kwao, hivyo Zahera na wenzako rekebisheni hili suala mapema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad