Zahera Awaingiza Chaka Waarabu
0
October 22, 2019
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amesema kuwa hahofii kutazamwa na wapinzani wake Pyramids FC ya nchini Misri mara atakaposhuka uwanjani kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC.
Yanga inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo Jumanne kabla ya kucheza na Pyramids katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Tayari kikosi cha Yanga kipo Mwanza tangu Jumamosi asubuhi kwa ajili ya kujiandaa na michezo hiyo miwili muhimu ambayo anahitaji ushindi.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa mfumo atakaoutumia kwenye mchezo dhidi ya Mbao ni tofauti na atakaoutumia dhidi ya Pyramids huku akiwapa matumaini ya ushindi mashabiki wa timu hiyo.
Zahera alisema kuwa katika mchezo dhidi ya Pyramids, atatumia mifumo miwili ambayo ni wa kushambulia ndani ya wakati mmoja kulinda goli lao huku wakicheza soka la pasi fupi na ndefu za haraka wakati wakiwa na mpira.
Aliongeza kuwa wakiwa hawana mpira anataka wachezaji wake wote wakabe na wawe mbele ya mpira na siyo nyuma ya mpira wasiwape nafasi ya kumiliki mpira wapinzani wao.
“Tumejipanga kucheza kufuatana na wapinzani wetu tutakaokabiliana nao, tupo tayari kuanza kucheza na Mbao kabla ya kuwavaa Pyramids, michezo yote tutakayocheza mkoani hapa.
“Nafahamu wapinzani wetu wanatufuatilia kwa ukaribu, ninaamini ni lazima watautazama mchezo wetu dhidi ya Mbao kupitia video au njia nyingine, lakini kwangu hainipi hofu kabisa.
“Kikubwa wafahamu kuwa jinsi nitakavyocheza na Mbao ni tofauti nitakavyocheza na Pyramids, nina mifumo na mbinu nyingi za uchezaji na uzuri tayari nimeshawaona wakiwa wanacheza, hivyo sina hofu,” alisema Zahera.
Tags