Akamatwa na Kadi 23 za Benki Tofauti, Azisokomezea Ukeni
0
November 23, 2019
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Bi Halima Juma (23) Mkazi wa Chalinze kwa tuhuma za wizi wa fedha kwenye mashine za kutolea fedha (ATM).
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, picha halisi ni kama ifuatavyo:
Mnamo tarehe 25/10/2019 katika Kituo cha Polisi Mbagala Maturubai, mzee Ernest Mika Sakala, ambaye ni Ofisa Mwandamizi Mstaafu wa Jeshi la Polisi alitoa ripoti kwamba tarehe 23/10/2011 majira ya 10:00hrs alibadilishiwa kadi yake ya benki ya CRDB na kupewa ya mtu mwingine bila yeye mwenyewe kufahamu, wakati alipokwenda kutoa fedha kwa wakala wa benki hiyo ambaye anaendesha biashara yake maeneo ya Dar Live Mbagala Zakhem.
Kwamba siku mbili baadaye aligundua kuwa kadi ya benki aliyo nayo siyo yake, na alipokwenda kufuatilia benki ya CRDB Mbagala siku ya tarehe 25/10/2019 aligundua kuibiwa kwa fedha kutoka kwenye account yake kiasi cha tzs. 10,000,000/=.
Fedha hizo zilitolewa kwa mawakala watatu tofauti siku ya tarehe 23 na 24 October, 2019. Upelelezi wa shauri hili ulianza kufanyika, ambapo mawakala ambao fedha zilitolewa na baadhi ya maafisa wa benki walihojiwa. Pia CCTV footages zilizomuonyesha mtuhumiwa wa kike aliyeonekana kutoa fedha kwa kutumia kadi hiyo iliyoibiwa kutoka kwa wakala mmoja wapo.
Wakati upelelezi ukiendelea, tarehe 19/11/2019 katika benki ya CRDB Mbagala wakala mmoja akiwa katika maeneo ya benki hiyo alimtilia shaka dada mmoja aliyeonekana kwenye ATM za benki hiyo akijaribu kutoa fedha, na alipomsogelea na kuanza kumuhoji dada huyo alijaribu kukimbia, lakini aliweza kudhibitiwa.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa na askari wanaolinda Benki hiyo na alipopekuliwa alikutwa na ATM kadi 23 za watu mbalimbali za benki tofauti tofauti zikiwa katika pochi yake huku akiwa amezificha katika sehemu zake za siri ukeni. Mojawapo ya kadi alizokutwa nazo ni ya mzee Ernest Mika Sakala. Kadi hizo zipo katika mchanganuo ufuato:
1. CRDB – kadi 07
2. NMB – kadi 06
3. NBC – kadi 02
4. Amana – kadi 02
5. Posta- kadi 02
6. ACB – kadi 01
7. Stanbic – kadi 01
8. DTB – kadi 01
9. Equity – kadi 01
Katika mahojiano, mtuhumiwa huyo ameeleza kwamba yeye na watuhumiwa wenzake, ambao bado tunawafuatilia, wamekuwa waki-target watu wenye umri mkubwa (wazee) na wastaafu ambao huenda kwenye mashine za ATM na kushindwa kuzitumia hivyo kuomba msaada kwa mtu wa pembeni.
Kwamba wakati wanapowasaidia kutoa fedha, kwa kutumia ujanja wanakariri namba za siri, na baada ya kufanya muamala wanachukua kadi ya muhusika na kuificha, na kumueleza kuwa kadi imemezwa kwenye mashine. Hivyo basi, victim anapoingia ndani ya benki kufuatilia kadi yake, wao wanaondoka na kadi kwenda kwa wakala yoyote yule au kwenye mashine nyingine ya ATM kuangalia salio na kuanza kutoa fedha.
Mbinu nyingine ni kuwafuatilia wateja wanaokwenda kutoa fedha kwa mawakala, na kukaa pembeni yao na kuchungulia pindi mteja anapoingiza namba yake ya siri.
Baada ya hapo mteja akishapewa fedha na wakala anakuwa busy kuweka mfukoni fedha alizopewa, huku kadi yake akiwa ameicha mezani, na hapo ndipo wanatumia mbinu ya kumbadilishia na kumuwekea kadi ya mtu mwingine ambayo tayari fedha zake wanakuwa walishaziiba. Amekana kushirikisha afisa yeyote wa benki au wakala katika kufanikisha wizi huo. Upelelezi bado unaendelea.
TAHADHARI YA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA JIJINI DAR ES SALAAM.
Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam linapenda kutoa tahadhari kwa wakazi wa jiji la Dsm wote kuwa makini kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepukana na majanga yanayoweza kuepukika.
Hivyo wananchi wote wanatakiwa kuwa makini na watoto wadogo wanaohitaji uangalizi wa karibu, pia kujiepusha kupita kwenye maji ya mito midogomidogo au madimbwi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao.
Aidha hadi sasa zimepokelewa taarifa za watu wawili kufariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Tags