Alinipiga Mpaka Kuniharibu Kizazi Kisha Akaniacha Kwasababu Siwezi Kumzalia


Tafadhali naomba ficha jina ila lakini naomba ushee kisa changu kwani naamini itasaidia wasomaji wako kujifunza kutoka kwangu. Mimi ni mwanamke wa miaka 27, niliolewa kama miama miwili hivi iliyopita na mwanaume ambaye tulidumu katika mahusiano kwa takribani miaka minne hivi kabla ya kufunga ndoa. Wakati tunakutana mimi nilikuwa chuo mwaka wa kwanza na yeye tayari alikuwa anafanya kazi.

Kusema kweli nilimpenda sana mume wangu kabla na baada ya ndoa na hata lakini kitendo alichonifanyia siwezi kukisahau katika maisha yangu. Mwanzo wa mapenzi yetu alikuwa mstaarabu sana, akinihudumia kwa kila kitu, akijali hisia zangu na kila mara kunionyesha kuwa ananijali na wakati wote tangu mwanzo alikuwa akisema kuwa mimi ndiye mwanamke ambaye angapenda kunioa.



Ingawa nilimpenda sana na alikuwa akionyesha kweli kuwa anamaanisha sikumuamini sana kwani nilijua wanaume wote ni waongo. Lakini kweli alionyesha kunipenda, tatizo lake alikuwa na wivu na hasira sana, yaani kila mara alitaka kuwa na mimi, hakutaka niwe na marafiki wa kiume. Kila rafiki aliyekuwa akiniona naye alihisi natembea naye na hilo lilinikwaza sana.

Nakumbuka wakati mmoja nikiwa niko ‘Discussion’ na wanafunzi wenzangu alinipigia simu nikachelewa kupokea, kwahiyo akawa amepiga kama mara mbili hivi, akaniuliza uko wapi nikamuambia nipo kwenye ‘discussion’ aliwasha gari na kuja mpaka chuo, alinikuta nipo na wakaka watatu ambao tulikuwa tunafanya ‘assigment’ alinichomoa katikati yao na kunipiga makofi mbele yao, kisha akanichukua mpaka kwenye gari lake na kuondoka na mimi.

Kitendo kile kilinikera sana kwani mbali na kuniumiza kimwili lakini alinidhalilisha pia, lakini nilikuja kumsamehe baada ya kuniomba sana msamaha. Madai yake iilikuwa kwanini niwe na ‘discussion’ na wanaume pekee, ukweli nikuwa group letu lilikuwa la watu sita wanaume watatu na wanawake watatu lakini rafiki zangu wawili walichelewa mjini hivyo sisi tukawa tumeamua kuendelea.

Hilo lilipita na kuahidi hatarudia tena, mambo yaliendelea vizuri akarudisha mapenzi lakini hakupunguza wivu, aliniminya sana mpaka kunifanya kuwatenga marafiki zangu wengi ili tu kumridhisha kwani sikutaka migogoro na yeye. Pamoja na yeye kuwa na wivu namna hiyo na kunichunga sana lakini mara kadhaa nilifumania meseji za wanawake wake wengine katika simu yake na nilipomuuliza ulikuwa ugomvi ambao ulipelekea hata kunipiga.

Kwasababu hiyo niliamua kutokumuuliza, hata nilipomkuta na mwanamke katika mazingira tata nilijifanya kipofu kwani nilimpenda sana na nilivumilia nikiamini kuwa iposiku atabadilika. Baada ya kumaliza chuo nilipata kazi hivyo kitu ambacho kilikuwa kimebakia ilikuwa ni ndoa tu. Kusema kweli nilikuwa na hamu sana ya ndoa kwani nilikuwa nikimpenda sana na kubwa kabisa nilijua baada ya kuoana atabadilika.

Niliamini kuwa baada ya kuniweka ndani hatakuwa na wivu tena na hatakuwa akinipiga kwani tayari atakuwa akinimiliki. Kichwani nilikuwa nikiamini sababu za wivu wake nikutokana na upendo wake kwangu na hofu ya kunipoteza, niliamini baada ya ndoa itakuwa rahisi kwangu kumbadilisha.

Niliongea naye kuhusu ndoa lakini aliniambia nisubiri “Unaharaka gani ya kuolewa?” Lilikuwa ndiyo jibu lake na kwakuwa nilimfahamu kama mtu wa hasira basi nilikaa kimya ili nisimuuzi. Siku moja nilichelewa kidogo kutoka kazini na wakati naondoka mfanyakazi mwenzangu ambaye yeye alikuwa na gari na alikuwa akikaa mtaa wa jirani na nilipokuwa nimepanga aliamua kunipa lifti.

Mara kadhaa hunipa lifti lakini anapofika kwake hunishusha na mimi kutembea kwa miguu mpaka kwangu kwani hakukuwa mbali sana, lakini siku hiyo kwakua nilichelewa sana aliamua kunifikisha mpaka getini. Alinishusha na kuondoka zake, niliingia ndani nikakuta mlango haujafungwa nikajua tu mpenzi wangu yuko ndani kwani alikuwa na funguo zangu na alikuwa na kawaida ya kuja bila taarifa.

Nilipoingia tu nikiwa sina hili wala lile nilikutana na kofi ambalo lilifuatiwa na teke lilionidondosha chini, kabla hata sijajiuliza ni kitu gani mtu alinikanyaga mguu na nikasikia ‘kaaaa’ mguu ulikuwa umevunjika. Hakujali aliendelea kunipiga kisha akaondoka kwa hasira, wakati akinipiga alikuwa akinitukana kuwa mimi ni Malaya na nimefikia hatua wanaume wangu wananileta mpaka nyumbani.

Aliniacha pale nikiwa katika maumivu makali, nilijaribu kunyanyuka lakini nilishindwa, kwa bahati nzuri kumbe wakati ananipiga majirani walisikia na alipotoka kwa hasira walimuona na waliposikia nalia kwa maumivu waliingia ndani na kuniona katika ile hali wakaamua kunipeleka hospitalini kwa kunipitishia Polisi kwanza. Ingawa nilikataa kupitia Polisi nikihofia kuwa mpenzi wangu atafungwa lakini waligoma wakisema siwezi kutibiwa bila PF3.

Kweli mguu ulivunjika nikafungwa POP, kule Polisi baada ya kuandika maelezo walitaka kufungua kesi lakini niligoma kutoa ushirikiano, hiyo ni baada ya kuniomba msamaha na kunivalisha pete nikiwa bado hospitalini. Ndugu zangu walinisihi sana kuachana naye lakini sikusikia, aliniambia ni shetani alikuwa amempitia na nilimuamini, aliomba msamaha sana akiahidi kubadilika.

Baada ya mimi kutokutoa ushirikiano na yeye kutoa pesa Polisi kesi ilifutwa kabisa na nikiwa bado na POP langu alijitambulisha kwetu rasmi ingawa walikuwa wanamjua akatoa mahari na mipango ya ndoa ikaanza kufanyika. Kama miezi minne hivi mguu ulishapona vizuri nikaweza kutembea bila msaada wa magongo na mwezi wa tano baada ya kile kipigo tulifunga ndoa.

Miezi ya mwanzo ya ndoa yetu ilikuwa mitamu na haikuchukua muda sana ndoa ilijibu, nilipata ujauzito kitu ambacho kilizidisha furaha, akawa mtu wa furaha, akapunguza wivu na hakukuwa na vipigo tena. Nilimshukuru Mungu kwa mabadiliko yale kwani nilikuwa na furaha tena na mume wangu alikuwa akijua kujali kwa vizawadi, outing za kutosha na vacation za hapa na pale.

Kusema kweli mambo yalikuwa mazuri mpaka mimba ilipofikisha miezi minne, hapo ndipo alipobadilika na kuanza kusema kuwa hataki nifanye kazi, mara ofisi yenu ina wanaume wengi, wivu ukarudi na kelele zikawa haziishi. Nilimgomea kuacha kazi kwani sikutaka kuwa Mama wa nyumbani, isitoshe kazi yenyewe ni nzuri na ina maslahi makubwa hivyo sikuona sababu ya kuacha kazi na kubaki kuwa mama wa nyumbani.

Mwanzoni sikujua nikwanini suala la kucha kazi limekuja ghafla wakati hapo awali alikuwa haliongelei, lakini nilipokuja kuchunguza ndipo nilipogundua kuwa kumbe alikuwa akitembea na dada mmoja pale ofisini kwetu na hakutaka mimi nijue ndipo akaona nibora niache kazi.

Siku moja wakati mimba ikiwa na kama miezi mitano hivi alikumbushia suala la mimi kucha kazi. Ingawa sikutaka kuzungumzia kuhusu yule dada kwani namjua hasira zake na nilishakubali kuishi naye hivyo hivyo hata kama anachepuka lakini nilipandwa na hasira na kuamua kumpasha ukweli kuwa sababu za kutaka mimi kuacha kazi ilikuwa ni yule dada wa ofisini.

Huwezi amini ilikuwa ni kama mimi ndiyo ninachepuka, aliwaka na kuanza matusi, alinitukana sana, kwakuwa najua hasira zake niliamua kukaa kimya na hilo pia lilikuwa kosa, alianza kunipiga akisema kuwa nina dharau, alinipiga sana sehemu mbalimbali bila kujali kuwa nilikuwa mjamzito, mimi sikufanya chochote kila mara nilijikunja ili kuzuia kupigwa tumboni.

Baada ya kumaliza kunipiga alinichukua na kwenda kunifungia stoo kisha yeye akaenda kulala. Kusema kweli nilipatwa na maumivu makali ambayo katika maisha yangu nilikuwa sijawahi kuyapata hasa eneo la tumbo na chini ya kitovu, damu zilianza kutoka na hapo ndipo nilijua kuwa nimempoteza mwanangu, nilijaribu kupiga kelele kumuambia mimba imetoka lakini hakusikia mpaka asubuhi ndipo alinifungulia.

Alinikuta nikiwa nimeshapoteza fahamu, mabonge bonge ya damu yapo chini. Alinichukua kunipeleka hospitali lakini kwa uoga alinipeleka katika kliniki tu ya rafiki yake ambaye alimuambia kuwa mimba imetoka, nilisafishwa na bila kumuambia mtu yeyote alinirudisha nyumbani. Siku nzima alikuwa akiniomba msamaha lakini sikuwa tayari kumsamehe, kila nilipowaza mtoto wangu hasira zilinipanda nakuwa mtu wakulia tu.

Wiki nzima alinihudumia yeye mwenyewe, nilianza kupata nafuu, sikumuambia mtu yeyote hata ndugu zangu kwani walishanikataza kuolewa na yule mtu, kuhusu mimba niliwaambia tu nilidondoka ghafla na mimba ikatoka. Wiki mbili baadaye nikiwa bado nyumbani kwakuwa kazini walijua mimba yangu imetoka tumbo lilianza kuuma tena, zamu hii kwa nguvu zaidi na vitu vyeusi kama uchafu kuanza kunitoka ukeni.

Nilimpigia mume wangu ambaye alikuja na kunikuta nimezidiwa, alinirudisha kwa yule yule daktari wake ambapo nilikaa huko siku mbili na hali ilipokuwa mbaya zaidi ndipo aliponipeleka Muhimbili, aliwambia kuwa nilipata ajali mimba ikatoka nakwenda kusafishwa, waliponichunguza ndipo waliposema kuwa nilisafishwa vibaya na kizazi kuguswa na kilishaoza ndiyo maana natokwa na uchafu na maumivu.

Hawakuwa na namna zaidi ya kukitoa kabisa na kunisafisha kwani kilishaharibika sana. Ilikuwa ni huzuni sana, nililia na kuzimia mara tano baada ya zile habari. Ndoto yangu ya kuwa Mama ilikuwa imesishia pale, mume wangu alijaribu kunituliza na kunifariji lakini haikusaidia, alinipa moyo kuwa alikuwa akinipenda mimi na si mtoto lakini wapi bado niliumia na sikuwa na mtu wa kumuambia maumivu yangu.

Nilikaa hospitalini kwa wiki moja na nilianza kujisikia vizuri kimwili nikaruhusiwa, nilitamani kuachana na mume wangu lakini nilishindwa. Kuna mambo mawili ambayo yalinizuia, kwanza ilikuwa ni namna ya kuwaambia ndugu zangu sababu za kuachana na mume wangu wakati walijua kuwa ndoa yetu inafuraha na kilichotokea ni ajali tu ya kawaida, hasa ikizingatiwa hawakujua kwamba nimepoteza kizazi.

Pili niliwaza ni mwanaume gani angeweza kunioa hasa akijua kuwa siwezi kumpatia mtoto? Nilijua kuwa hakuna mwanaume ambaye angeweza kunivumilia tofauti na mume wangu hasa ikizingatiwa kuwa yeye ndiyo alinisababishia lile tatizo. Nilivumilia na maisha yaliendelea furaha ilirejea kwa muda mchache mpaka nilipogundua kuwa amempa mimba  mwanamke mwingine tofauti kabisa na yule wa ofisini.

Nilinyamaza tu kwani nilijua kama ningeongea ingeleta shida, ingekuwa kipigo isitoshe sikutegemea kama angekaa tu na mimi bila kutafuta mtoto sehemu nyingine, hata mimi nilitamani awe na mtoto nilitamani kulea na nilijipa moyo kama angenileteea basi ningemlea bila kinyongo chochote. Lakini haikuwa hivyo bila ugomvwi wowote bila kutegemea siku moja  tu aliniambia.

Siwezi kuishi na mwanamke ambaye hazai, nimevumilia lakini nimeshindwa, sasa hapa kwangu utakuwa unafanya nini? Kungekua na shida nyingine labda mirija imeziba tungehangaika pamoja ila huna kizazi na huwezi kupata mtoto, tutaishi hivi mpaka lini. Mimi tayari nina mtu ana mimba yangu hivyo anataka kuja kuishi humu.

Najua nimechangia wewe kuwa hivyo lakindi ndiyo ishatokea sina chakufanya, siwezi kukurudishia kizazi chako lakini pia siwezi kukudanganya kuwa sitaki mtoto, namhitajisa na na nahitaji kuwa na familia. Mimi naona tu uondoke, sinakinyongo na wewe lakini siwezi kuishi na wewe tena, siwezi kuigiza tena.

Aliongea taratibu sana, macho yake yalionyesha kuwa alikuwa anamaanisha alichokuwa akikiongea na hakuwa tayari kurudi nyuma. Nnilimuangalia mara mbili nikajua hakuna kitu ambacho ningesema kitakachoweza kubadilisha maamuzi yake. Nilijikuta nasema tu “Sawa” basi sikuonge aneno lolote, hata alipotaka kugawana mali, sijui kunipa gari na vitu vingine nilimuangalia tu.

Akili yangu nika ilifunga, sikutaka kuchukua chochote. Siku iliyofuata nilikusanya kila kitu nilichokuwa nimenunua na hela yangu na kuondoka, alijaribu kunisihi tugawane kila kitu lakini nilikataa, nilitaka kuanza maisha yangu upya bila yeye. Sasa hivi naishi mwenyewe na nina jaribu kutafuta furaha tena, sihitaji tena mwanaume najikita kwenye kazi.

Tupo kwenye mchakato wa talaka rasmi ya kiserikali, ndugu hawajui sababu lakini wanahisi tu labda yeye ndiyo alinipiiga ingawa nawakatalia. Nimeamua kumsamehe kwaajili ya amani yangu mwenyewe na namuombea Mungu furaha katika mahusiano yake mapya, namuombea mwanamke mwenzangu yasijekumkuta kama yangu na naamini kama ana akili amejifunza hawezi kupiga mwanamke tena.

Najua siwezi kuzaa lakini hiyo haimaanishi kuwa siwezi kuwa Mama, kuna watoto yatima wengi wapo mitaani wanatafuta wazazi na mipango yangu sasa ni kutafuta pesa ili nikifikisha miaka 33 niwe na nyumba yangu na maisha mazuri ya kuweza kulea watoto wawili ambao nina mpango wa ku wa ‘adopt’ kuwa wangu kabisa.

Kuhusu wanaume nadhani kwa sasa sina hisia kabisa, nikiwaona nawaona kama wanawake wenzangu tu, siwachukii lakini sina hamu nao. Sababu ya kuamua kushea maisha yangu ni ili mabinti wadogo wajifunze kuwa huwezi tu kumbadilisha mtu tabia, vumilia kila kitu ila kama anakupiga usivumilie, usiingie kwenye ndoa ukadhani unaweza mbadilisha mwanaume ni ngumu, mwanaume hubaidlika pale anapoamua kubadilika yeye mwenyewe.

Najua unapokuwa katikati ya mapenzi huoni, macho hufungwa na kujipa moyo kwa kuangalia mazuri yamwenza wako ila usiwe kipofu kuona yaliyowazi. Ana wanawake wengi unamvumilia tena anakuonyesha na haoni kama ni kitu kibaya, anakupiga unavumilia, siku akikuvunja mguu au kukupa ulemavu wa kudumu ndipo utajutia kama mimi atakucha kwakuwa hutakuwa na vigezo ulivyokuwa navyo awali vilivyomfanya akupende.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. admin naomba umpe email yangu please musajmkama@gmail.com

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad