Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) limemfungia kwa miaka kumi (10) aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Jamal Malinzi baada ya kumkuta na hatia ya matumizi mabaya ya fedha na kughushi nyaraka.
Mbali na adhabu hiyo, Malinzi pia amepigwa faini ya CHF 500,000 za Uswisi ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 1.1 za Kitanzania, baada ya uchunguzi wa Kamati ya Maadili ya FIFA uliobaini kuwa Malinzi alihusika katika matumizi mabaya ya fedha za FIFA (FIFA Financial Assistance Programme (FAP) funds), fedha za CAF.
Matumizi mengine aliyohusishwa ni fedha za TFF pamoja na kughushi nyaraka za maazimio ya Kamati ya Utendaji ya TFF kati ya mwaka 2013 na 2017.
Adhabu hiyo inaanza kufanya kazi kuanzia Novemba 8, 2019 na tayari Malinzi mwenyewe ameshajulishwa.
“Kamati imemkuta na hatia ya kuvunja kanuni ya 24 inayohusu kughushi nyaraka, na kanuni ya 28 inayohusu matumizi mabaya ya fedha katika kanuni za maadili ya FIFA toleo la mwaka 2018 na hivyo inamfungia miaka kumi kujihusisha za shughuli zote za soka Kitaifa na Kimataifa”, imeeleza sehemu ya taarifa iliyotolewa leo na FIFA.