Baada ya Harmo Kusepa, Utata WCB Kulipwa Mil 500
0
November 24, 2019
NYUMA ya zile shilingi milioni mia tano (500) ambazo staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ alidai kuilipa lebo ya muziki iliyomlea kisanaa ya Wasafi Classic Baby (WCB) ili kuvunja mkataba nayo, zimezua utata, Ijumaa limedokezwa.
Agosti 21, mwaka huu, mmoja wa mameneja wa Lebo ya Wasafi iliyo chini ya mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Salam SK alitangaza Harmonize au Harmo kuandika barua ya kujitoa kwenye lebo hiyo.
Baada ya hapo, Harmo naye alieleza jinsi ambavyo alikuwa akijisikia raha moyoni baada ya kuvunja mkataba na Wasafi uliomgharimu kiasi cha shilingi milioni 500 kisha kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide.
“Nimelazimika kuuza nyumba zangu tatu ili kuwalipa Wasafi na kuvunja nao mkataba na sasa ukweli ni kwamba sina uhusiano mzuri na lebo hiyo,” alisema Harmonize.
UTATA WA NYUMBA
Jambo la kwanza ambalo Gazeti la Ijumaa lilitia shaka na kutaka uthibitisho ni juu ya Harmo kumiliki nyumba tatu jijini Dar ambapo lilianzia uchunguzi wake kwa watu wake wa karibu.
“Ninachojua Harmonize ana nyumba moja tu, ipo Madale (Tegeta) na ni ya ghorofa moja ambayo hata hivyo, haijakamilika.
“Hizo nyingine kwa kweli sizijui na kama angekuwa ameuza nyumba hivi karibuni ningejua,” alisema mtu wa karibu wa Harmo aliyeomba hifadhi ya jina na kuongeza;
NI VIGUMU KUAMINI
“Mimi mwenyewe nilishtuka kusikia ameuza nyumba tatu hapa mjini. Unajua ni vigumu kwa mtu kuamini kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu au minne tayari ana nyumba tatu mjini, zenye thamani ya shilingi milioni 500, labda angesema amekopa au amekubaliana na Wasafi kuwa atawalipa kidogokidogo.
BILA MAPICHAPICHA?
“Kwanza mimi ninavyowajua Wasafi na hata Harmonize, wasingeweza kufanya kitu kama hicho halafu kusiwe na mapichapicha.
“Kama ni kweli wangekuwa wamemwaga documents (nyaraka) za mikataba hadharani.”
IJUMAA MADALE
Hata hivyo, Gazeti la Ijumaa lilifika kwenye nyumba ya Harmo ambayo haijamalizika iliyopo Madale jijini Dar na kuzungumza na mlinzi wake.
Mlinzi huyo alilithibitishia gazeti hili kuwa Harmo anamiliki nyumba hiyo moja na kwamba haijauzwa kwani yeye angejua kwa kuwa ndiye mlinzi wa nyumba hiyo.
“Tumesikia watu wakisema nyumba imeuzwa ili alipe gharama za kuvunja mkataba, lakini siyo nyumba hii. Nawahakikishia haijauzwa!
“Kwanza namuomba Mungu isiuzwe kwa sababu hapa ndipo ninapopatia mkate wangu wa siku,” alisema mlinzi huyo.
SERIKALI ZA MITAA
Gazeti la Ijumaa lilifika kwenye Ofisi za Serikali ya Mtaa wa Mivumoni- Madale jijini Dar, ilipo nyumba hiyo ambapo mwenyekiti alikanusha Harmo kuuza nyumba hiyo.
“Labda kama kuna nyingine, lakini hii haijauzwa. Haiwezekani ikauzwa bila Serikali ya mtaa huu kujua.”
MAMENEJA WASAFI
Ili kujua kama kweli Wasafi walilipwa kiasi hicho cha pesa, Gazeti la Ijumaa liliwatafuta mameneja wa Wasafi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’, Said Fella ‘Mkubwa’ na Sallam SK.
Kwa upande wao, Babu Tale na Sallam simu zao ziliita bila kupokelewa, lakini alipotafutwa Fella alifunguka anachokijua.
Fella alisema hana maelezo kamili juu ya Harmonize kulipa shilingi milioni 500 kwani hawajakaa kikao cha ishu hiyo.
“Sina maelezo kamili kwa sababu hatujakaa kikao. Hapo katikati tulikuwa bize na Tamasha la Wasafi, lakini ngoja nilimuulize Sallam SK atakachonijibu nitakwambia au unaweza kuongea naye pia,” alisema Fella.
Hata hivyo, walipotafutwa kwa mara nyingine, Babu Tale na Sallam SK bado hawakujibu chochote hivyo jitihada zinaendelea ili kujua mbivu na mbichi juu ya pesa hizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ aliahidi kulifafanua jambo hilo atakapotulia. Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni hakuwa amefafanua.
Stori: Mwandishi Wetu, Ijumaa
Tags