Baada ya Vyama Vya Upinzani Kujitoa, Serikali Yasema Uchaguzi Serikali za Mitaa Uko PalePale


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uko pale pale na utafanyika Novemba 24, 2019 kama ilivyopangwa licha ya vyama vingine kujitoa kwenye Uchaguzi huo.

Jafo ameyasema hayo mapema leo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Ofisini kwake Jijini Dodoma kuhusu maendeleo ya  maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea uongozi sambamba  na Kamati za Rufaa.

Alisema zoezi la uchukuaji wa urejeshaji wa fomu za kugombea uongozi limeenda vizuri na wananchi waliochukua fomu ni 555,036 na waliorejesha ni 539,993 sawa na asilimia 97.29 ya wananchi wote waliochukua fomu, na ambao hakurejesha ni asilimi 2.7 tu.

“Hii inaonyesha muamko mkubwa wa wananchi kutaka kuongoza katika ngazi ya Serikali za Mitaa na mchakato mzima wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulienda vizuri ukiwa na Kanuni bora zaidi  kulinganisha na chaguzi zilizotangulia” alisema Jafo.

Aliongeza kuwa baada ya zoezi hili kukamilika lilifuatiwa na uteuzi ambao ulilenga kuteua wagombea wenye sifa, waliokidhi vigezo na kufuata taratibu zote za ujazaji wa fomu za kugombea na kubandiwa kwa orodha ya wagombea waliopitishwa katika hatua hiyo.

Wagombea pia walipata fursa ya kuwasilisha pingamizi zao kwa mujibu wa Kanuni na kisha kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa za Wilaya zilizoundwa kwa ajili ya kuratibu rufaa za wagombea alisema Jafo.

Waziri Jafo alifafanua kuwa mpaka hivi sasa rufaa zilizowasilishwa kutoka kwenye vyama mbalimbali vya siasa ni 13,500 na zinafanyiwa kazi na Kamati za Rufaa za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo zoezi hilo litakamilika leo hii Tarehe 09/11/2019.

Akizungumzia baadhi ya vyama kujitoa kwenye Uchaguzi ilihali wanachama wao walishateuliwa amma kuwasilisha rufaa zao kwenye Kamati  alisema kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi jina la mgombea likishateuliwa linabaki kwenye karatasi za kupigia kura siku ya Tarehe 24/11/2019 hata kama chama chake kimejiengua kushiriki kwenye Uchaguzi .

Aliendelea kuelezea kuwa wakati zoezi la uteuzi na kamati za rufaa zikiendelea na kazi yake alipata fursa ya kufanya ziara katika mikoa ya Singida, Manyara, Dododma,Iringa na Njombe ambapo  alijionea baadhi ya makosa yaliyofanywa na wagombea wakati wa ujazaji wa fomu lakini pia alizungumza na Kamati za Rufaa.

Alitaja makosa yaliyobainishwa kwenye fomu za wagombea kuwa ni  “Kujaza umri mdogo kuliko umri unaostahili kwa mgombea, sehemu ya tarehe kuweka sahihi au mtu kuchukua fomu na kujidhamini mwenyewe au majina kutofautiana wakati wa kujiandikisha kwenye orodha ya mpigakura na kwenye fomu ya kugombea hivyo Wasimamizi walifanya kazi yao kwa mujibu wa miongozo na Kanuni za Uchaguzi” Alisema Jafo.

Lakini bado nafasi ilikuwepo endapo mgombea  angeona hakuteuliwa kwa kuonewa ipo Kamati ya Rufaa ambayo ingeweza kuskiliza malalamiko ya mgombea na kuyafanyia kazi alisisitiza Jafo.

“Kuanzia kesho tutaanza kutoa Taarifa ya Rufaa zilizopita na watu walioteuliwa kushiriki uchaguzi huo kupitia Kamati za Rufaa " alimalizia Waziri Jafo
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad