Bibi Amuangukia Rais Magufuli
0
November 18, 2019
BIBI Halima Athuman (78), mkazi wa Manzese-Uzuri jijini Dar, amemwangukia Rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’, akimuomba amsaidie kwani kuna mtu anataka kumdhulumu nyumba yake. Akizungumza na Gazeti la Ijumaa Wikienda akiwa kitandani nyumbani hapo Manzese-Uzuri, bibi Halima alidai mtu huyo anayetaka kumdhulumu nyumba hiyo ni mumewe ambaye alifunga naye ndoa mwaka 1962.
“Niliolewa na huyo mwanaume mwaka 1962. Katika maisha yetu tulijaaliwa watoto tisa, lakini wanne wamefariki dunia. “Niliishi naye kwenye nyumba za kupanga ambapo tulianzia Kisutu kisha Jangwani. “Baadaye tulifanikiwa kupata eneo hili la Manzese-Uzuri ambalo tulilinunua kwa shilingi 150 mwaka 1972.
“Tulijikusanya huku mimi nikiwa nauza vitumbua hadi tukafanikiwa kujenga nyumba tatu, maana eneo hili lilikuwa ni kubwa.“Mwaka 1996, mume wangu alioa mke mwingine na baadaye akaongeza mwingine tena.
“Hapo ndipo tatizo lilipoanzia maana alikata mawasiliano na mimi na watoto wangu. “Nilihangaika mwenyewe na watoto hadi wakakua. Baadaye mume wangu aliamua kuuza nyumba mbili bila kunishirikisha, ikabaki nyumba moja ambayo vyumba vitatu na hao wake wenzangu wamepewa vyumba na vyumba vingine wanakaa wapangaji ambapo mimi sipati hata shilingi.
“Kilichonishangaza zaidi ni kitendo cha mume wangu kuja kuniambia anipe shilingi milioni nane ili niondoke kwenye nyumba yangu ambayo niliitolea jasho langu ili aiuze. “Siwezi kuondoka kwenye nyumba yangu kwa sababu ni jasho langu na yeye ameshauza nyumba mbili bila kunipa hata shilingi moja. “Ilibidi niende Serikali za Mitaa ambapo kesi yetu ilisikilizwa, tukaambiwa twende wilayani (Kinondoni).
“Kule wilayani nilikutana na mwanasheria, akanisikiliza ndipo mume wangu akaambiwa yeye ameshauza haki yake hapa palipobaki ni kwangu. “Pamoja na kuambiwa hivyo, mume wangu ameendelea kushinikiza kuuza nyumba na kutishia kunitupia vitu nje.
“Nimeshaenda kwa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, lakini sijafanikiwa kumzuia. Hivyo, namuomba Rais Magufuli anisaidie nipate haki yangu,” alisema Halima ambaye ni mgonjwa mwenye hali mbaya. Ijumaa Wikienda lilimtafuta mwanaume huyo ambaye alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwani lipo kiserikali. Alipotafutwa Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, simu yake iliita bila kupokelewa
Tags