SIMBA wameshtuka na wameamua kubadilisha aina ya mazoezi kwa nahodha wao, John Bocco ikiwa ni sehemu ya kumrejesha uwanjani straika huyo baada ya kuwa nje kwa zaidi ya miezi mitatu.
Benchi la ufundi la Simba chini ya kocha wake mkuu Mbelgiji Patrick Aussems kwa sasa limekuja na mbinu ya kumpunguzia mazoezi ya muda mrefu Bocco kwa kuwa mazoezi hayo ndiyo yanachangia hadi sasa kutoonekana uwanjani.
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, ameliambia Championi Jumatatu kuwa Bocco kwa sasa atakuwa anafanya mazoezi kwa muda mfupi kwa kuwa mazoezi ya muda mrefu yanampa maumivu ambayo yanamchelewesha kupona majeraha yake.
“Kwa sasa Bocco amepunguziwa mazoezi na atakuwa anafanya mazoezi kwa muda mdogo kwa sababu akifanya hivyo anapata maumivu ambayo yanamchelewesha kupona hadi sasa licha ya kwamba anahitajika ndani ya timu.
“Tumeona mazoezi ya muda mrefu yanachangia kumfanya hadi sasa ashindwe kurejea ndani ya timu na plani ambayo iko mbele ni hiyo, atafanya mazoezi kwa muda mchache chini ya uangalizi wa madaktari wa timu,” alisema Rweyemamu