MTENDAJI Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amefunguka kuwa kiungo wa klabu hiyo, Jonas Mkude ana uwezo wa kucheza ligi yoyote duniani endapo tu ataacha masuala ya utovu wa nidhamu.
Kauli hii inakuja baada ya kiongozi huyo kusema wachezaji wengi wa Bongo wanashindwa kucheza soka Afrika Kusini kutokana na kutokuwa na nidhamu tu.
Mazingisa alifunguka zaidi kuwa wachezaji kadhaa wa Simba wana uwezo wa kucheza soka Afrika Kusini endapo tu wakipata nafasi hiyo.
Kiongozi huyo, alisema suala la nidhamu limekuwa ni tatizo kwa wachezaji wengi ndiyo maana imekuwa ikiwagharimu kwa kiasi kikubwa na kushindwa kufanya vizuri.
Mtendaji huyo alisema mchezaji kama Mkude ana uwezo mzuri sana akiwa uwanjani, endapo akitulia na kuacha utovu wa nidhamu nje ya uwanja atakuwa bora zaidi.
“Wachezaji wengi wa hapa Tanzania wanashindwa kwenda kucheza soka Afrika Kusini kwa sababu ya suala la nidhamu ndiyo linawafelisha wengi.
“Mkude ana uwezo wa kucheza ligi ya Sauzi, lakini siyo Sauzi tu, ila ana uwezo wa kucheza popote pale sababu uwezo anao ila anatakiwa kuacha mambo mengine ya nje ya uwanja.
“Pale anapocheza anakuwa halali kwa wakati, hapumziki muda unaotakiwa na hafanyi mazoezi vizuri lakini unamuona vile, jaribu kuangalia kama angekuwa anafanya kila kitu kwa nidhamu ingekuwaje?
“Lakini kuna wachezaji wa Simba ambao wana uwezo wa kucheza Sauzi ni pamoja na Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Sharaf Shiboub, Meddie Kagere ana uwezo wa kucheza Sauzi ila umri tayari umekimbia, ila akicheza atafanya vizuri,” alisema Mazingisa.