Patrick Aussems, kocha mkuu wa Simba ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji ametangaza hali ya hatari kwa wapinzani wa Simba ambao atakutana nao kwenye mchezo wao unaofuata wa ligi.
Aussems aliondoka nchini Tanzania Jumatatu ya wiki hii kimyakimya na kurejea nyumbani kwao Ubelgiji kwa kile alichokieleza kuwa ni kutokana na sababu zake binafsi na aliahidi kurejea jana akiwa na hasira za kupata pointi tatu za Ruvu Shooting iliyo nafasi ya nane na ina pointi 15. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Aussems amesema:”
"Niliondoka kwa sababu zangu binafsi mwenyewe kwa siku mbili nitarejea kesho (jana), kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Ruvu Shooting nazihitaji pointi tatu.
” Championi Jumatano, lilizungumza na Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ambaye alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala la kocha kwa kuwa bosi wao ameshazungumza.
“Bosi amesema kuwa hajui alipo kocha sasa mimi nitazungumza nini hapo, zaidi ya kufuata kile ambacho amesema CEO? (Mkurugenzi Mtendaji) basi kwa kuwa mwajiri hajui alipo mfanyakazi wake hakuna nitakachoweza kuzungumza,” alisema Rweyemamu.
Simba inatarajiwa kushuka Uwanja wa Uhuru Novemba 24 kumenyana na Ruvu Shooting mchezo wao wa 10 kwenye ligi ikiwa nafasi ya kwanza baada ya kucheza mechi 9 na imejikusanyia pointi 22, imepoteza mchezo mmoja mbele ya Mwadui FC na imeshinda mechi saba na sare moja dhidi ya Prisons