Bwege "Atema Nyongo", Asema Vyama vya Upinzani Visimtafute Mchawi



Na Ahmad Mmow,  Lindi.

Mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini, Selemani Bungara ( Bwege) ametoa wito vyama vya siasa vya upinzani nchini viache kulalamika na kupiga kelele dhidi ya yanayoendelea dhidi yake. Kwani havina wa kumlaumu.

Bwege ameyasema hayo leo, alipozungumza na Muungwana Blog baada ya kuombwa atoe maoni yake kuhusu malalamiko ya vyama vya upinzani baada ya wagombea wake wengi kuenguliwa kugombea nafasi za uenyekiti wa mitaa, vijiji na vitongoji na ujumbe wa serikali za mitaa na vijiji.

Alisema vyama vya upinzani havina sababu ya kulalamika wala kupiga kelele. Kwani yaliyofanyika dhidi yake ni matokeo ya ubinafsi baina ya vyama hivyo. Hali ambayo itasababisha vishindwe kushika dola kwa miaka mingi toka sasa.

Alisema kilichotokea ni zao la upinzani baada ya kushindwa kushirikiana ili viwe na umoja wenye nguvu na kuweza kupigania demokrasia na mfumo wa vyama vingi nchini. Badala yake kila chama kinafanya mambo kivyake. Hali ambayo pia inasababisha vishindwe kuwa na sauti ya pamoja.

" Tumeshindwa kupaza sauti zetu kwapamoja wakati  demokrasidola na mfumo wa vyama  vingi vya siasa unatelekezwa. Vyama ambavyo vipo kwa mujibu wa katiba na sheria namba tano ya vyama vya siasa. Hususani kuzuiliwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa," alisema Bwege.

Kutokana na hali hiyo, Bwege alisema vyama hivyo visitegemee kuwepo chaguzi huru na haki. Kwamadai kwamba kutegemea kushinda kwenye chaguzi hizo ni sawa na mtu anayetamani kufika peponi wakati anaogopa kufa. Huku akijua njia ya kufika peponi ni kifo.

Bwege ambaye ni maarufu ndani na nje ya bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisema vyama hivyo visimtafute mchawi. Kwani vinajiroga vyenyewe kwa sababu vina ubinafsi, woga na usaliti baina yake. Mambo ambayo yamesababisha vifike vilipo sasa.

Alisema udhaifu wa vyama vya siasa vya upinzani unatumiwa vema na chama kilichounda dola. Kwahiyo badala ya kuendelea kulalamika havinabudi vijitafakari na vichukue hatua ya kujisahihisha.

" Kwakuwa tumeshindwa kulienzi na kulisimamia Azimio la Zanzibar, tutambue kwamba upinzani Tanzania kushika dola ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano," Bwege alisisitiza.

Katika hali iliyoonesha mbunge huyo machachari aliamua kutoa ya moyoni alisema kwakuwa vimeshindwa kushirikiana ili viwe na umoja wenye nguvu wakati vinajua kwamba ushirikiano ni jambo lililo ndani ya uwezo wake. Kwahiyo kushiriki chaguzi vikitegemea kushinda ni sawa na kutwanga maji.

" Hatuwezi kufikia lengo letu kuu la kushika dola. Bali vitaishia kupata ruzuku ya vyama toka serikalini tu," Bwege alitahadharisha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad